Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

UKATILI:Mtoto Achinjwa Kama Kuku Tandika Azimio Jijini Dar

Marehemu, Abdul Karim (pichani) mwenye umri wa miaka minne.
  
UMESHAWAHI kushuhudia mtu akichinja kuku? Kama jibu ni ndiyo, basi ndivyo anavyoonekana kufanyiwa kitendo hicho mtoto Abdul Karim (pichani) mwenye umri wa miaka minne wa Tandika Azimio jijini Dar baada ya kiwiliwili chake kuokotwa kikiwa hakina kichwa, Ijumaa lina habari hii ya kusikitisha.
NI BAADA YA KUPOTEA KWA SIKU 3
Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Juni 9, mwaka huu baada ya kupotea katika mazingira ya kutatanisha Juni 7, hali iliyowafanya wazazi, ndugu na majirani wachanganyikiwe na wasijue la kufanya.
SIKIA SIMULIZI YA KUUMA YA MAMA
Akizungumza na Ijumaa kwa uchungu, mama wa mtoto huyo, Maimuna Khamis alisema; “Siku ambayo mwanangu alipotea, ilikuwa majira ya saa 12 jioni, nilitoka kwenda dukani kununua kibiriti, Abdul nikamuacha na baba yake na mtoto mdogo.
“Wakati niko dukani, yule mtoto mdogo akawa analia sana hivyo mume wangu akamtuma Abdul aje kuniita, alimtuma kwa kuwa nyumbani na dukani siyo mbali sana. “Alipotumwa na baba yake alinikuta njiani nikiwa narudi kutoka dukani hivyo nikachukua hela, nikampa akanunue dawa ya mbu kwani nilikuwa nimesahau. “Baada ya kumpa ile pesa kisha mimi kuwahi nyumbani, tulikaa sana bila kumuona Abdul akirudi, ndipo jitihada za kumtafuta zikaanza. Tulizunguka kila sehemu mpaka saa saba usiku hatukufanikiwa kumuona. Hapo ndipo tukaanza kuchanganyikiwa na kwenda kutoa taarifa misikitini na kwenye kituo cha polisi.
Mama yake mzazi Abdul Karim.
BAADA YA SIKU 3
Mama huyo alieleza kuwa, tangu siku ambayo mtoto huyo alipotea, kila kukicha wamekuwa wakihangaika kumtafuta lakini jitihada hazikuzaa matunda hadi Juni 7, mwaka huu walipopata taarifa zilizowafanya wauamini ule msemo usemao, dunia ni katili.
“Siku ya tatu tulipata taarifa kuwa, kuna mtoto kaonekana katupwa eneo la Kaburi Moja lakini mwili hauna kichwa. Niliishiwa nguvu nilipopata taarifa hizo. Sikutaka kabisa kwenda kuuona mwili maana nilijua kuwa, na mimi ningeweza kufa kwa presha.
“Watu walivyoenda akiwemo baba yake, waligundua kuwa ni mwanangu na alikuwa kweli amechinjwa kama kuku, kama mzazi nimeumia sana, mwanangu ambaye nilikuwa nampenda sana na nilitamani siku nimuone anakuwa mkubwa, nimeumia sana tena sana…” alisema mama huyo huku machozi yakimtiririka. Aliongeza kuwa, walibaini kuwa mwili ulikuwa ni wa Abdul kutokana na kwamba alikuwa amevaa kaptura aliyotoka nayo siku alipopotea lakini pia alikuwa na ‘hogo’ (P.O.P) alilofungwa kwenye mkono baada ya kuumia siku zilizopita. “Ulikuwa ni msiba mzito kwa familia, mwanangu ameuawa kikatili….hakuwa na kosa lolote, inauma sana. Baada ya kuuona mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Temeke ambapo ulifanyiwa uchunguzi kisha tukakabidhiwa na kwenda kuuzika,” alisema mama huyo.
Waombolezaji wakiwa na simanzi kwenye msiba wa mtoto huyo.
MAJIRANI WANASEMAJE?
Wakizungumza na Ijumaa kwa nyakati tofauti, baadhi ya majirani walieleza kusikitishwa na tukio hilo la kinyama na kuomba vyombo husika kufanya uchunguzi na kubaini wauaji.
“Kwa kweli ni tukio ambalo kila mtu linamtoa machozi, tunajiuliza malaika yule kawakosea nini mpaka wanamchinja vile kama kuku? Mungu anawaona na adhabu kubwa wataipata,” alisema Sule Karim wa Tandika.
Naye mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Mama Sadick alisema kuwa, wameshindwa kujua kuwa waliofanya tukio hilo walikuwa na dhamira gani hadi kuamua kumchinja mtoto huyo na kuondoka na kichwa. “Kwa kweli tumebaki na maswali mengi, ni ushirikina au kitu gani? Lakini kwa kuwa tunaamini mtoto wa watu hakuwa na kosa, Mungu anajua cha kuwafanya waliomuua,” alisema mama huyo.
Ijumaa baada ya kupata taarifa hiyo lilifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke jijini Dar, Gilles Muroto ambapo kila alipopigiwa simu yake haikupokelewa kabla ya baadaye kueleza kuwa, atafutwe wakati mwingine kwani alikuwa ‘taiti’.
Hata hivyo, tukio hili liwe fundisho kwa wazazi kuwa makini sana na watoto wao wanapokuwa mbali na nyumbani kwani hata Jeshi la Polisi nchini chini ya IGP Simon Sirro limekuwa likihimiza kila mmoja kuwa sehemu ya usalama wa familia na taifa kwa ujumla. Gazeti hili linaipa pole familia ya mtoto Abdul na tunamuomba Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. Inna Lillah, Wainna Ilaih Rajiuun.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017