Wengi wetu tumekuwa tukitafuta mbinu za kuishi maisha mazuri na kwa muda mrefu katika dunia hii ambayo kila kitu sasa ni hatari kwa afya.
Wenye bahati ya kuepuka madhara ya kemikali zinazosababisha saratani, mbu wa malaria, Ukimwi, ajali au kuuawa kwa tuhuma za uchawi, huishi miaka kati ya 50 au 70.
Wako wachache wanaofikisha umri wa kuanzia miaka 90 au 100 na kuendelea na wanapatikana kwa nadra.
Lakini Damalis Chilemela, anayeishi Veternary, Temeke amevuka yote hayo na sasa ana umri wa miaka 120 uliomuwezesha kuona wajukuu 31 na vitukuu 47.
Na hadi wakati Mwananchi inaongea naye, uso wake ulikuwa unapambwa kwa furaha, lakini mwenye kupenda kuimba na kucheza na kama ilivyo kwa wazee wengine, ananusa ugoro ambao humsababishia apige chafya.
Damalis, aliyezaliwa mwaka 1897, kwa sasa anaishi na mtoto wake wa nne katika eneo la Veternary wilayani Temeke.
Si kwamba umri wake umemfanya apoteze kumbukumbu, la hasha. Damalis anakumbuka hata mwaka aliozaliwa na baadhi ya matukio yaliyotokea zamani pengine wakati huo zaidi ya robo tatu ya watu waliopo dunia walikuwa hawajazaliwa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, alizaliwa kijiji cha Mwadwa kilichopo wilaya ya Chamwino, Dodoma.
Damalis alisema alifanikiwa kupata watoto 14 na kwa bahati mbaya, ni watoto watano kati ya hao ndiyo wapo hai kwa sasa.
“Sasa hivi nimechukuliwa na watoto wangu nipo hapa Dar es Salaam naishi na mtoto wangu wa nne baada ya kufiwa na mume wangu mwaka 2013,” alisema.
Alisema mume wake alifariki akiwa na umri wa miaka 99.
“Mume wangu alikuwa mdogo kwangu kiumri,” alisema ajuza huyo.
Siri ya kuishi miaka 120
Kwa jinsi wanasayansi wanavyozungumzia magonjwa yanayosababishwa na vyakula tulivyozoea kula, ni dhahiri swali kuhusu mlo wake haliwezi kuepukika.
“Kwa kawaida nimekuwa nikila ugali wa mtama, uwele na mboga kama maharage, mlenda na majani ya kunde,” anasema Damalis.
“Nilikuwa nakunywa zaidi maziwa halisi ya ng’ombe ambayo nakamua mwenyewe.”
Chile Chilemela, mtoto wa Damalis, alisema tangu akiwa mdogo hadi sasa hakuwahi kumuona mama yake akila mboga aina ya dagaa na samaki wakati wakiwa kijijini.
“Vyakula alivyokuwa akila vimemsaidia sana. Ninachokumbuka, katika maisha niliyoishi na mama yangu, sijawahi kumuona akisumbuliwa na magonjwa mengine zaidi ya homa ndogondogo na meno ambayo yalikuwa yakimuuma,” alisema Chilemela.
Alisema baada ya kuletwa Dar es Salaam, mfumo wa maisha yake umebadilika kutokana na mazingira kwa kuwa amelazimika kuacha kula vyakula alivyokuwa akitumia kijijini.
“Sasa hivi hachagui chakula, anakula kwa kujilazimisha. Kama mboga za majani hali kabisa hadi zitoke kijijini,” alisema.
“Tangu afike mjini ni nyama na samaki zikikosekana hizo anataka apikiwe maharage.
“Tangu aanze kula vyakula vya huku tulishangaa hivi karibuni akidai kuwa akitembea anachoka sana na tulipompeleka kwa daktari alituambia ana presha ya kushuka.”
Mambo anayokumbuka
Kitu cha kustaajabisha ni jinsi ajuza huyo anavyokumbuka matukio makubwa ya kihistoria kama vita ya majimaji iliyotokea mwaka 1905 -1907.
“Wakati huo nadhani nilikuwa na miaka kati ya minane na kumi, kwa sababu niliona watu wanashikwa ili waende kupigana vita ya majimaji,” anasema.
“Nakumbuka kipindi hicho Mtemi alikuwa anapiga baragumu kwa kutumia pembe la mnyama kwa kuwataarifu watu wawe na tahadhali kuwa vita vinaendelea.”
Bibi huyo alisema wanaume walikuwa wanakamatwa kwa ajili ya kupelekwa kwenye vitani.
Wajukuu 31 na vitukuu 47
Chilemela, mtoto wa Damalis alisema mama yao alikuwa watoto 14.
Alisema kwa bahati mbaya baadhi wamefariki na kwa sasa wamebaki watoto watano.
Aliongeza kuwa watoto ambao wako hai ni Samweli mwenye miaka 71, Jeremia (65), Habel (63), Aidan (59) na Job (47).
Kwa upande wa wajukuu alisema wako 31 kati ya hao 18 wa kiume na wa kike 13. Pia, Damalis amebarikiwa kupata vitukuu 47.
Daktari wa magonjwa ya binadamu wa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, Kanani George alisema kwa umri alionao bibi huyo ni busara zaidi asile vyakula ambavyo vinaweza kumuweka katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Alisema ndugu zake wanapomuandalia chakula bibi huyo wanatakiwa kumumuwekea chumvi kidogo na kumshauri asitumie kilevi chochote kwa kuwa kinaweza kumsababishia shinikizo la damu, moyo na hata saratani.
Agosti 2016, wakati Dorothy Chandler Collins wa Marekani aliposherehekea miaka 100 ya kuzaliwa, aliwapa binti na wajukuu wake wa kike siri ya kuishi maisha marefu kuwa ni kukaa mbali na wanaume.
Taifa lenye wananchi wengi waliojaliwa kuishi maisha marefu ni Japan.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini