
Majeruhi Tabia Mbonde akiuguza majeraha aliyoyapata kutokana na kushambuliwa.
INATISHA sana! Hii ni simulizi ya mwanamke ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Rwaruke, Kibiti mkoani Pwani, Tabia Mbonde ambaye ameshuhudia mumewe, Ramadhani Mzuzuri akiuawa mbele yake kisha naye kumiminiwa risasi tano baada ya kuvamiwa na watu wanaodhaniwa kuwa miongoni mwa kundi linaloendeleza mauaji maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, Risasi Jumamosi lina mkasa nzima.
Baada ya kutokea tukio hilo, mapema wiki hii, wanahabari wetu walifika kijijini hapo kisha kumfuata Tabia aliyelazwa kwenye Hospitali ya Mchukwi iliyopo Songa, Kibiti ambaye alianika simulizi nzito ya jinsi walivyovamiwa hadi mumewe kuuawa na yeye kujeruhiwa kwa idadi hiyo ya risasi.
SIKIA SIMULIZI HII
Huku akiugulia maumivu makali akiwa wodini hospitalini hapo, Tabia alisema kuwa, siku ya tukio, majira ya usiku, wakiwa wamepumzika, walishtukia wamevamiwa na watu wenye silaha waliokuwa wakimhitaji mumewe Ramadhani.
“Walikuja na (Toyota) Noah nyeupe mpaka karibu na nyumba yetu kisha wakavamia nyumba na kuvunja mlango.

Ramadhani Mzuzuri enzi za uhai wake.
“Baada ya kuvunja mlango, walikutana na mimi uso kwa uso. Niliwaona watu watatu warefu waliokuwa na silaha na hapo nikajua kabisa kuwa tulikuwa tumeshavamiwa.
“Waliniuliza kama mume wangu alikuwepo, nikawaambia hayupo.
“Nilipowajibu hivyo walionekana kutoniamini na kwamba walikuwa na uhakika kuwa yupo hivyo walianza kunipiga ngumi na mateke.
“Walikuwa wakiniambia kuwa wataniua kwa kujitakia mwenyewe kwani wao hawakuwa na shida na mimi, lakini kwa kuwa nilionekana kutowapa ushirikiano, walisema lazima waniue.
“Wakati hayo yote yakitokea mume wangu alikuwa chumbani na alikuwa anasikia tunavyolumbana.
MUMEWE AJIFICHA DARINI
“Alichokifanya mume wangu kwa kujua kabisa kuwa watu hao hawatamuacha hai, alipanda darini kujificha akidhani angeinusuru roho yake lakini pamoja na jitihada zote hizo umauti ulimkuta (kilio cha kwikwi).
“Baada kuona wanazidi kunitesa pale mlangoni, niliwaponyoka na kuanza kuwakimbia lakini kabla sijafika mbali walinimiminia risasi mfululizo zipatazo tano ambapo zilinijeruhi miguu yote.
Tabia Mbonde akionyesha majeraha yake.
“Risasi nyingine ilinipiga kutokea nyuma kwenye ubavu wa kulia na kunitoboa titi kama hivi mnavyoniona (akionesha jeraha la risasi kwenye titi).
“Walipoona hilo halitoshi, waliendelea kunikimbiza hadi kwenye kichaka kilicho karibu na nyumba yetu ambapo waliendelea kunipiga risasi nyingine.
“Baada ya kunipiga risasi nyingi na hasa ile waliyonipiga ubavuni, waliona siwezi kupona tena hivyo wakaamini nimekufa na nilimsikia mmoja wao akiwaambia wenzake huyo tayari twendeni ndani tukamtafute mumewe,”alisimulia Tabia huku akieleza kuwa alikuwa akishuhudia kila kitu wakat i mumewe akiuawa kwani alikuwa akiona na kusikia lakini hakuwa na uwezo wa kusimama au kupambana.

Afisa Tawala Hospitali ya Mchukwi, Yasinta Maneno.
RISASI ZARINDIMA KWA SAA 2
Tabia aliendelea kusimulia kwamba, tukio hilo lilichukua zaidi ya saa mbili huku risasi zikirindima, lakini katika hali ya kustaajabisha hakukuwa na msaada wowote kwani wanakijiji waliogopa.
“Wale wauaji, baada ya kuona wameshanimaliza walimrudia mume wangu na kuanza kumtafuta mle ndani. Kumbe alikuwa amejificha darini.
“Katika kutafuta niliwasikia wakisema kuwa wamemuona ndipo wakaanza kumshambulia kwa risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Walianza kummiminia risasi akiwa mlemle darini kabla ya kumshusha na kuendelea kumpiga risasi. Mume wangu alikuwa akijitahidi kujiokoa lakini ulifika muda akadondoka mlangoni na nikamshuhudia akikata roho.

…Akizungumza na Global TV Online.
“Pamoja na kwamba nilikuwa na maumivu makali, lakini siwezi kusahau ile picha ya mume wangu kukata roho. Inauma sana, nadhani kwa wanawake wenzangu wanajua maumivu ya zaidi ya uchungu.
“Huo ndiyo ukawa mwisho wa uhai wa mume wangu na hadi nipo hapa hospitalini sijui chanzo ni nini kwa sababu hatujawahi kupata hata vitisho vya aina yoyote,” alisema Tabia, mama wa watoto wawili aliozaa na mumewe huyo akiwemo wa miezi mitatu aliyekoswakoswa na risasi na kuongeza: “Namshukuru Mungu nimepata matibabu tangu nilipoletwa hapa usiku ule nikiwa katika hali mbaya na mume wangu ameshapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.”

SACP Onesmo Lyanga.
KAMANDA WA POLISI SASA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji (Mkiru), SACP Onesmo Lyanga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba oparesheni maalum ya kuwasaka wahalifu hao inaendelea.
Mpaka sasa zaidi ya watu 35 wamepoteza maisha kwenye matukio ya mauaji katika wilaya hizo huku Jeshi la Polisi likiwa limejipanga vilivyo kukomesha tatizo hilo.
Kuangalia zaidi mahojiano ya mama huyu ingia youtube kisha andika globaltvonline usisahau kusubscribe.
STORI: WAANDISHI WETU | RISASI JUMAMOSI
====
SHUDUHIA MAMA HUYO AKIFUNGUKA
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini