Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Magufuli Amtwanga Barua Kali Waziri Mkuu Canada Kuhusu Bombardier..Lazima Ziachiwe


Dar/Bukoba. Rais John Magufuli amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau akimtaka ashughulikie kwa haraka suala la ndege ya Bombadier Q400 inayoshikiliwa nchini humo.
Ndege hiyo ni miongoni mwa ambazo Rais John Magufuli aliahidi kununua ikiwa ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ilitarajiwa kuwasili nchini Julai mwaka huu lakini hilo halikufanyika na Agosti 18, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema ndege hiyo imekamatwa nchini Canada na inaweza kupigwa mnada kutokana na deni ambalo Serikali inadaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ya Montreal, Canada.
Kampuni hiyo iliishtaki Serikali katika Mahakama ya kimataifa, ikipinga kuvunjiwa mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo, jijini Dar es Salaam ambayo ilitaka kulipwa fidia ya Dola 38 milioni za Marekani, sawa na zaidi ya Sh87 bilioni.
Akizungumza katika uzinduzi wa Uwanja wa ndege mjini Bukoba jana, Rais Magufuli alisema licha ya kuandika barua kwa Waziri Mkuu wa Canada, amemtuma Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini humo kushughulikia suala hilo kisheria.
“Nimemwandikia barua waziri wa Canada kuulizia ni kwa nini ndege yetu inakaa zaidi ya miezi sita... pia nimemtuma mwanasheria akapambane kisheria,” alisema.

Atengua uteuzi wa wakurugenzi
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na mwenzake wa Bukoba Vijiji, Mwantumu Dau ambao watapangiwa kazi nyingine.
Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara zilizopokewa kwenye halmashauri zao walipoulizwa swali hilo wakati wa uzinduzi wa uwanja huo na Rais aliwaambia kuwa amewasamehe kabla ya baadaye jioni Ikulu kutoa taarifa ikieleza kutenguliwa kwa uteuzi wao.
Alipoitwa kufika mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi cha fedha zilizopokewa kwenye halmashauri kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara, Mwantumu alijibu kuwa ana idara nyingi anazozisimamia hivyo si rahisi kwake kukumbuka kila kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina akisema hawezi kusema uongo kauli ambayo ilionekana kumkera Dk Magufuli.

Neema kwa watumishi yaja
Akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua uwanja huo, Rais Magufuli alisema Sh159 bilioni zitatumika kulipa malimbikizo ya stahiki za watumishi wa umma kuanzia mwezi ujao lakini akaagiza uchunguzi dhidi ya watumishi watatu wa Serikali waliopitisha malipo hewa ya Sh15.2 bilioni.
Pamoja na watumishi hao, aliwataja Jackson Kaswahili, Mwachano Ramadhani na Gideon Zakayo, akisema baada ya uhakiki imebainika kiasi cha fedha wanazodai si sahihi.
Rais Magufuli alisema Kaswahili aliandika kuwa anaidai Serikali Sh7.62 bilioni, Ramadhani Sh1.75 bilioni na Zakayo Sh104 milioni.
Bila ya kutaja wizara au idara wanakotoka serikalini, Rais pia aliagiza watumishi 110 waliowasilisha madai hewa wachunguzwe.
Ameagiza vyombo vya dola kuwachunguza mara moja watu hao aliowataja na walioidhinisha madai yao.
Awali, Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Rwekatare alimuomba Rais Magufuli kuwezesha ujenzi wa soko la kisasa akisema viongozi wa Bukoba wakiwamo madiwani wa vyama vyote, wana mshikamano katika masuala ya maendeleo bila kujali tofauti zao za kiitikadi.
Usipitwe na Habari Muhimu, Install App  Yetu


Android ===>  Bofya hapa
Alimkumbusha Rais kuhusu uwepo wa waathirika wa tetemeko la ardhi la Septemba 10, 2016 wanaohitaji misaada.
Wabunge wa CCM waliokuwapo na kupewa nafasi ya kuzungumza na majimbo yao kwenye mabano ni Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini), Dk Deodorus Kamala (Nkenge) na Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini).
Profesa Tibaijuka aliomba reli ya kisasa itakayojengwa kwenda nchini Rwanda ichepushwe hadi Bukoba ili kusaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera.

Uwanja wa ndege
Awali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Richard Mayongela alimweleza Rais kuwa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba umegharimu Sh31.9 bilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh6.3 bilioni zimetolewa na Serikali na Sh25 bilioni zimetolewa na Benki ya Dunia (WB). Aliiomba Serikali kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuhudumia miundombinu ya viwanja vya ndege nchini.

Barabara za lami Muleba
Awali, akiwa njiani kuelekea Bukoba Rais Magufuli alizungumza na wananchi wilayani Muleba na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Emmanuel Sherembi kutumia fedha za Mfuko wa Barabara kujenga barabara za mji huo kwa kiwango cha lami ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Aliwaahidi wakazi wa wilaya hiyo kuwa atatekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ya kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 26 za barabara kutoka mjini Muleba hadi Hospitali ya Rubya.
Aliwaagiza viongozi wilayani humo kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji na kulinda mazingira katika Hifadhi ya Burigi kwa kuhakikisha mifugo kutoka nchi jirani inayoingia nchini kinyemela inadhibitiwa.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017