Kuendesha gari ni suala linalohitaji umakini na utulivu mkubwa. Haijalishi unaendesha mjini au unaendesha kijijini kote kunamuhitaji dereva kuwa makini ili yeye, gari, abiria aliowabeba, pamoja na watumiaji wengine wawe salama.
Linapokuja suala la kuendesha gari umbali mrefu, hapa umakini unatakiwa kuongezeka maradufu. Wapo madereva wengi ambao wamezoea kuendesha magari mijini lakini siyo kwa safari ndefu. Unapokuwa na safari ndefu (wengi huziita safari za mkoani) wewe kama dereva inakubidi kuongeza umakini hata kama umezoea kuendesha gari kwa muda mrefu.
Mara kwa mara kumeshuhudiwa ajali mbalimbali ambazo kimsingi zinatokana na madereva kutokuzingatia kanuni muhimu katika utumiaji wa vyombo vya usafiri.
Ili kuhakikisha usalama wako pamoja na watumiaji wengine wa barabara, yapo mambo kadhaa unayopaswa kuyazingatia kabla na wakati wa kuendesha gari umbali mrefu.
Kagua na andaa gari
Kabla ya safari yoyote gari linahitaji kukaguliwa na kuandaliwa, hasa kabla ya safari ndefu. Kuna mambo kadhaa unayohitaji kuyakagua kwenye gari lako na kuhakikisaha kuwa yako sawa kama inavyopaswa:
- Kagua hali na ubora wa magurudumu. Hakikisha magurudumu yana upepo kwa kiwango kinachohitajika na hayajaisha muda wa matumizi yake.
- Kagua mafuta lainishi (oil). Hakikisha gari yako ina mafuta lainishi ya kutosha tena yenye ubora unaotakiwa.
- Kagua kiasi cha kipoozeo cha injini (Coolant) japo wengine huweka maji. ‘Coolant’ ni muhimu sana kwenye gari kwa ajili ya kupooza injini ya gari.
- Kagua utendajikazi wa injini. Hakikisha injini yako inafanya kazi vizuri.
- Kagua sehemu nyingine za gari kama vile breki, kiongeza mwendo (accelerator), usukani, taa, honi, viashiria (indicators), n.k.
- Hakikisha maji ya kusafishia kioo yapo ya kutosha. yatakusaidia kusafisha kioo chako pale kitakapochafuka.
Hakikisha unalikagua gari lako vyema na kuliandaa kwa ajili ya safari. Unaweza pia kumtumia mtaalamu wa magari ili akusaidie kulikagua na kuliandaa kwa safari yako.
Pata muda wa kutosha wa kupumzika
Ili uweze kuendesha gari vyema wakati wa safari ndefu ni muhimu kupumzika kwa kiasi cha kutosha kabla na wakati wa safari.
Hakikisha kabla ya safari unapata muda wa kutosha wa kulala ili kuepusha kusinzia barabarani kunakoweza kusababisha ajali. Unapokuwa barabarani unaweza pia kupumzika baada ya umbali fulani ili usichoke sana.
Kumbuka kupumzika uwapo safarini kutakuwezesha kupata nguvu zaidi na kutoa nafasi ya gari lako kupoa ili kuepusha ajali ya gari kuwaka moto.
Fahamu kuhusu hali ya hewa
Safari yako inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa. Hivyo ni vyema ukahakikisha unafahamu hali ya hewa ya eneo unalokwenda ili ujiandae mapema.
Kwa mfano kama kunatarajiwa kunyesha mvua, ni vyema ukachunguza kama barabara utakayoitumia kama huwa inapitika wakati wa mvua ili usije ukakwama. Unaweza kutumia vyombo vya habari au mtandao wa Google ili kufahamu hali ya hewa ya eneo unalokwenda.
Beba vitu muhimu
Kama ilivyo ada, safari inahitaji maandalizi. Hakikisha unabeba vitu muhimu unavyoweza kuvitumia kwenye safari yako kama hivi vifuatavyo:
- Chakula na vinywaji. Ikiwa hutonunua chakula au kupata mahali pa uhakika pa kununua chakula na vinywaji, basi beba chakula chako utakachokula mara uwapo safarini.
- Beba kisanduku cha huduma ya kwanza. Ni muhimu kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza kwenye gari ili upatapo tatizo la kiafya kikusaidie.
- Beba vifaa vya msingi vya matengenezo ya gari. Vifaa kama vile jeki, spana, tochi, n.k. ni muhimu sana.
Tumia mafuta vizuri
Hakikisha unatumia mafuta vizuri mara uendeshapo gari umbali mrefu ili kuhakikisha unapunguza gharama zisizokuwa za lazima. Hakikisha pia huachi kiwango cha mafuta kipungue sana ili usije ukaishiwa mafuta kwenye eneo ambalo liko mbali na kituo cha mafuta.
Fuata sheria na kanuni
Kuna kanuni zinazotawala matumizi ya barabara pamoja na vyombo vya usafiri. Ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, hakikisha unafahamu vyema sheria za barabarani za eneo unalokwenda. Beba vibali na nyaraka muhimu za dereva na gari Mf. leseni, bima, pia kama utavuka mipaka ya nchi beba pasi ya kusafiria pamoja na Visa kama inahitajika.
Endesha mwendo salama
Mwendokasi ni chanzo kikubwa cha ajali na matatizo mengi barabarani. Ni muhimu kuendesha gari kwa mwendo wa wastani ili kuepusha matatizo yasiyokuwa na ulazima. Kumbuka! Unapoendesha gari kwa mwendo wa wastani ni rahisi kujihami mara kunapotokea tatizo barabarani.
Usitumie Kilevi chochote unapoendesha
Chanzo kikubwa cha ajali ni ulevi au matumizi ya pombe kwa madereva. Pombe hukufanya ushindwe kumudu gari vyema, hivyo usitumie kilevi kabla na wakati wa safari.
Zingatia Burudani
Burudani tena? Ndiyo, unaweza kuweka miziki ambayo itakuburudisha wewe pamoja na wale unaosafiri nao ili msichoke muwapo safarini. Kusikiliza mziki wakati wa kuendesha gari kutakuweka katika hali (mood) nzuri sana.
Ni dhahiri kuwa yapo manufaa kadha wa kadha yatokanayo na kusikiliza mziki. Ni wazi kuwa mziki huboresha na kuweka afya za miili na akili zetu katika hali nzuri.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini