Upande wa utetezi wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow juzi ulimbana shahidi wa 15 wa upande wa mashtaka kueleza tofauti kati ya ufunguo wa pikipiki na wa gari.
Kesi hiyo namba 192 ya 2014 inawakabili washtakiwa saba wanaotetewa na mawakili saba inasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, mbele ya Jaji Sirilius Matupa.
Shahidi huyo ambaye ni balozi wa nyumba 10 katika Mtaa wa Nyanshana, Kata ya Mbugani jijini Mwanza, Biseko Mgeta (53) alibanwa na mawakili wa upande wa utetezi baada ya kumaliza kuulizwa maswali na upande wa Jamhuri.
Katika maelezo yake shahidi huyo alieleza jinsi alivyoshuhudia mmoja wa washtakiwa alivyoingia kwenye shimo la choo mara tatu kuopoa Radio Call, betri yake na ufunguo wa gari uliokuwa umeandikwa Toyo.
Mahojiano ya shahidi huyo na mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na James Njelwa yalikuwa kama ifuatavyo:-
Wakili: Una elimu gani?
Shahidi: Nimesoma mpaka darasa la saba.
Wakili: Mwanzoni umeileza mahakama kuwa vitu vilivyoopolewa kwenye choo ni redio call, betri yake na ufunguo wa gari, si ndiyo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Una utaalamu wa vifaa vinavyohusiana na mambo ya redio na ulisomea wapi?
Shahidi: Sina.
Wakili: Je una utaalamu wowote kuhusu magari?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Ulisema awali kuwa kwenye tukio hilo la Novemba 3, 2012 ulisaini nyaraka ngapi? Ikumbushe mahakama.
Shahidi: Mbili.
Wakili: Unaweza kuzitaja nyaraka hizo ulizosaini?
Shahidi: Ndiyo naweza.
Wakili: Zitaje?
Shahidi: Nyaraka ya upekuzi na maelezo yangu binafsi.
Wakili: Ulizisoma hizo nyaraka?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Unakumbuka ulichokisoma siku hiyo baada ya kuzisoma hizo nyaraka?
Shahidi: Nakumbuka ilikuwa imeandikwa hati ya upekuzi Nyanshana.
Wakili: Zilikuwa zimeandikwa kwa Kiswahili?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Ni vitu gani vilikufanya kugundua kuwa hii ni radio call na betri yake?
Shahidi: Askari ndiye aliyesema hivyo na mimi nikafahamu.
Wakili: Hiyo radio call ilikuwa imeandikwaje?
Shahidi: Motorola.
Wakili: Ikumbushe mahakama kuwa ufunguo wa gari uliotolewa kwenye shimo la choo ulikuwa umeandikwaje?
Shahidi: Ulikuwa umeandikwa Toyo.
Wakili: Unajua kuwa kuna pikipiki inaitwa Toyo?
Shahidi: Ndiyo nafahamu.
Wakili: Je, kuna gari inayoitwa Toyo?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili: Unajua kusoma?
Shahidi: Kingereza au?
Wakili: Kiswahili?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo utakubaliana nami kuwa ufunguo huo ulikuwa ni wa pikipiki inaitwa Toyo?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili aliomba kibali cha Mahakama kumpatia shahidi hati ya upekuzi ili aisome kuonyesha neno lililoandikwa Toyo.
Wakili: Hebu soma kwa sauti hiyo hati ya upekuzi?
Shahidi: (Alisoma hati hiyo ambayo pamoja na mambo mengine ilikuwa imeandikwa vitu vilivyotolewa chooni ni pamoja radio call, betri na ufunguo wa gari aina ya Toyota)
Wakili: Kwa hiyo neno Toyo lipo wapi?
Shahidi: Nimekosea kidogo.
Wakili: Ni ufunguo upi kati ya ule wa gari na wa pikipiki ni mrefu zaidi?
Shahidi: Sijawahi kutumia gari mimi najua tu wa pikipiki.
Shahidi : Uliwaona watuhumiwa wakitupa vitu hivyo ndani ya choo?
Shahidi : Sikuwaona.
Wakili: Ulijuaje kama ndio waliotupia vitu hivyo ndani?
Shahidi: Baada ya kuambiwa na askari waliokuwapo eneo la tukio wakiwa wamewafunga pingu mikononi.
Wakili: Hizo karatasi ulizosaini zilikuwa zimeandikwa hati ya upekuzi?
Shahidi: Ndiyo, pale juu ile karatasi ilikuwa imeandikwa hivyo.
Wakili: Hebu tuonyeshe hilo neno kwenye hii karatasi uliyosaini kwa kipindi hicho?
Shahidi: (Alilitafuta neno hilo na kulikosa kwenye karatasi na wakili akaendelea kumuuliza kama analiona au aseme halipo, baadaye shahidi huyo akasema halipo).
Wakili: Ufunguo ulikuwa na rangi gani?
Shahidi: Nyeupe.
Wakili: Ulionyeshwa namba za radio call?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Hicho choo unachosema vitu hivyo vilitupwa nje kuna uzio au la?
Shahidi: Hakuna uzio.
Wakili: Choo hicho kipo karibu na njia?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo, kuna uwezekano wa watu wengine kutupa vitu hivyo kwenye hicho choo?
Shahidi: Ndiyo.
Awali, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Ajuaye Bilishanga kutoa ushahidi aliileza Mahakama jinsi alivyoshuhudia choo hicho kikibomolewa na mshtakiwa mmoja kuingia ndani ya choo kutoa ufunguo wa gari aina ya Toyo, radio call na betri yake.
Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:-
Wakili: Unaitwa nani?
Shahidi: Naitwa Biseko Mgeta.
Wakili: Una ishi wapi?
Shahidi: Naishi Nyanshana Kata ya Mbugani jijini Mwanza.
Wakili: Unafanya shughuli gani?
Shahidi: Nafanya kazi ya kuendesha pikipiki maarufu bodaboda.
Wakili: Unafanyia wapi kazi yako?
Shahidi: Nafanyia maeneo ya mjini kati na Nyanshana.
Wakili: Mbali na kazi ya bodaboda kazi gani nyingine unafanya?
Shahidi: Ni balozi wa nyumba 10 katika mtaa wangu.
Wakili: Novemba 3, 2012 mchana ulikuwa wapi?
Shaidi: Nilikuwa kwenye shughuli zangu za kila siku.
Wakili: Eleza Mahakama kilichotokea?
Shahidi: Nilipigwa simu na mke wangu Veronica Malimi akiniambia kuwa niende nyumbani kuna askari nyumba ya jirani yangu (Ikombe Pius) wananihitaji. Kwa muda huo nami sikuchelewa nikaondoka kwenda nyumbani.
Wakili: Ulipofika kwako nini kilitokea?
Shahidi: Mke wangu aliniambia niende kwa jirani Ikombe Pius (shahidi 14) kuna askari na muda huohuo kabla sijaondoka hata huyo jirani yangu akafika kunichukua.
Wakili: Endelea kuileza mahakama kilichotokea?
Shahidi: Baada ya hapo tuliongozana na huyo jirani kuelekea kwake.
Wakili: Mlipofika ulikuta nini?
Shahidi: Niliwakuta askari na watu wengine, ndipo mmoja wa askari akajitambulisha kwangu kuwa anaitwa afande (Joseph) Konyo na kuniambia kuwa kuna watuhumiwa wawili waliomuua kamanda wa polisi na kuna vitu walivitupa kwenye shimo la choo, hivyo wanataka nishuhudie vikitolewa.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Ilitengenezwa ngazi, mimi nikafuata reki nyumbani kwangu na fundi akabomoa mlango wa choo na mmoja wa watuhumiwa aliingia ndani na kuanza kuvitoa vitu hivyo kwa kutumia reki.
Aliingia mara ya kwanza akakorogakoroga akatoa radio call, mara ya pili akatoa betri na mara ya tatu alitoa ufunguo wa gari ulioandikwa Toyo.
Wakili: Nini kiliendelea baada ya kuvitoa vitu hivyo?
Shahidi: Waliviosha kwa maji na kuonekana vizuri na baada ya hapo niliandika maelezo na kuyasaini pamoja na karatasi ya upekuzi.
Shauri hilo liliahirishwa juzi na litaendelea Jumanne ijayo.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini