Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Simbachawene: Serikali Iliahidi Elimu Bila Malipo Na Si Elimu Bure


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, amefafanua suala la sera ya elimu lililoahidiwa na serikali ya awamu ya tano alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake Bungeni mjini Dodoma.
Hii ni baada ya kuwepo kwa mgogoro baina ya wazazi/walezi na shule za serikali kuhusu uhalali wa michango wanayochangishwa pamoja na serikali kuahidi kutoa elimu bure.
Waziri Simbachawene alieleza kuwa kuna tofauti kati ya elimu bure ya msingi na elimu ya msingi bila malipo, na kuwataka wananchi kutokuacha kushiriki katika michango mbalimbali inayohusu elimu kwa kisingizio kwamba serikali imeahidi kutoa elimu bure.
“Wananchi wanakuwa wazito kujitolea hata nguvu zao katika kuchangia shughuli mbalimbali zinazohusu elimu kwa kisingizio kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa elimu msingi bure,” alisema.
Aliendelea kwa kutoa wito kwa wadau wote wa elimu, Mamlaka za serikali, asasi zisizo za kiserikali pamoja na wazazi na walezi kushiriki katika kuimarisha miundombinu itakayowawezesha wanafunzi kupata elimu katika mazingira rafiki kupitia michango mbalimbali.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, asasi zisizo za kiserikali, wadau wengine wa elimu, wazazi na walezi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha uwepo wa miundombinu muhimu ya shule kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali, msingi na sekondari,” alisema.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017