Uteuzi wa Miss Tanzania namba mbili wa mwaka 2006, Jokate Mwegelo kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, unaonekana kutaka kuivuruga jumuiya hiyo.
Mjadala mkubwa umeibuka kuhusu uteuzi huo, ambapo baadhi ya wanachama na viongozi wa juu wa jumuiya hiyo wamedai kuwa haukufuata kanuni na taratibu za umoja huo.
Vyanzo vya kuaminika kutoka katika umoja huo vimedai kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa UVCCM hawakushirikishwa katika uteuzi huo uliofanywa na kigogo mmoja wa umoja huo.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa uteuzi huo haukushirikisha wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wala Baraza Kuu la UVCCM, ambalo halikukutana kumthibitisha Jokate kama kanuni zinavyoelekeza.
Kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, wajumbe wa kamati ya utekelezaji hawazidi 10, ambapo miongoni mwao ni Mwenyekiti wa umoja huo Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na mjumbe mmoja kutoka makao makuu ya chama.
Wajumbe wa baraza kuu ni wenyeviti na makatibu wa mikoa na mjumbe mmoja kutoka katika kila mkoa.
Kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni mvurugano ndani ya umoja huo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa uteuzi huo ulifuata taratibu zote za chama.
“Ni kweli amekaimishwa kwa kufuata taratibu zote za chama, kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilikutana Aprili 18, mwaka huu, Dar es Salaam na ndicho kimewakaimisha wakuu wa idara watano akiwamo Jokate.
“Hao wanaolalamika hawajui kanuni na taratibu za jumuiya yetu, huwezi kupata nafasi kama kikao cha Kamati ya Utekelezaji hakijakaa,” alisema Shaka.
Hata hivyo alikiri kutoitishwa kwa kikao cha Baraza Kuu ili kuthibitisha uteuzi huo, akisema ni gharama kubwa kuitisha kikao hicho.
“Kwa kawaida Baraza Kuu huwa linakutana kila baada ya mwaka mmoja, kuita baraza kuu ni gharama sana hivyo ikitokea kuna nafasi wazi Kamati ya Utekelezaji ina mamlaka pia ya kumthibitisha,” alisema.
Kwa upande wake, Jokate alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kuifanya jumuiya hiyo iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania.
“Nashukuru kwa imani waliyoonyesha viongozi wangu ila zaidi kuona nina uwezo wa kuongoza idara hiyo nyeti na muhimu kwenye jumuiya.
“Kikubwa ni kuifanya jumuiya iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania na kurudisha tumaini na kusimamia changamoto wanazozikabili vijana katika kujiletea maendeleo,” alisema Jokate.
Jokate pia alikuwa miongozi mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Jokate alianzia kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo aliibuka mshindi wa pili.
Hivi sasa anajishughulisha na sanaa na ujasiriamali ambapo anamiliki Lebo ya Kidoti Fashion inayojihusisha na uuzaji wa nywele na mavazi.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini