Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Wodi Ya Wazazi Muhimbili Yafurika Wengine Walazimika Kulala Chini

WODI ya wazazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili imefurika wagonjwa kiasi cha baadhi yao kulazimika kulala kwenye magodoro maalumu sakafuni.
Kutokana na hali hiyo, katika mitandao ya kijamii zimekuwa zikisambaa picha zikiwaonesha kina mama wakiwa wamelala chini na watoto wao (wachanga), huku mjadala mzito ukiibuka na wengine kuhoji kuhusu tukio hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa Muhimbili, Agnes Mtawa, alithibitisha kufurika kwa wagonjwa katika hospitali hiyo, hasa wodi ya wazazi ambayo ina uwezo wa kulaza watu 130 tu.
“Wodi yetu ina uwezo wa kulaza watoto wachanga 130 na wazazi wao 130, hivyo jumla yao ni 260, lakini hali huwa tofauti hasa inapofika kipindi cha Januari hadi Juni, kila mwaka idadi ya wazazi tunaopokea huongezeka mara dufu.
“Kwa mfano leo (jana) tayari tumepokea watoto wachanga 228 ambao wamezaliwa katika hospitali za rufaa, huwa wanaletwa huku wakiwa na matatizo mbalimbali kwa mfano kuchelewa kulala,” alisema Mtawa.
Alisema watoto hao wanapofikishwa hospitalini hapo mama zao hulazimika kuwa nao karibu na ndiyo maana wodi hiyo huonekana kujaa kila wakati.
“Nimeeleza awali kwamba uwezo wa wodi yetu ni kulaza watoto 130 pekee, kwa idadi hiyo ya wagonjwa 228 maana yake tuna ongezeko la watoto 98 wakati nafasi ikiwa ni ile ile,” alisisitiza.
Mtawa alisema hata hivyo hawajawahi kufanya utafiti wowote kujua kwanini wagonjwa wengi hufurika katika kipindi hicho cha kuanzia Januari hadi Juni ya kila mwaka.
Alisema watoto wengi waliopokea wanatoka katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro huku baadhi wakitoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Lakini ieleweke kwamba Muhimbili kwa ujumla haijafurika wagonjwa, tuna uwezo wa kulaza wagonjwa 1,500 na leo (jana) tumepokea wagonjwa 1,258 pekee, changamoto ipo kwenye wodi ya wazazi, tunashauri ili kukabili hali hii ni vema hospitali za rufaa zikaimarishwa, tunashukuru Serikali imeliona jambo hilo na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa,” alisema.
Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Kina mama na Uzazi wa hospitali hiyo, Dk. Vincent Tarimo, alisema kwa kuwa kipaumbele chao ni kuhudumia wagonjwa, huwa wanalazimika kuwapokea hivyo hivyo na si kuwarudisha nyumbani.
“Hatuwezi kuwarudisha, lazima tuwapokee tuwahudumie, ni kipaumbele chetu, Serikali iendelee kuweka nguvu zaidi kwenye hospitali za rufaa,” alisema.
credit:Mtanzania

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017