MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, amesema vitendo vya polisi kuwakamata waandishi wa habari wanapokuwa katika majukumu yao ya taaluma siyo msimamo wa jeshi hilo bali ni la bahati mbaya.
Alisema waandishi na vyombo vya habari ni wadau muhimu wa jeshi hilo lazima washirikiane nao.
IGP Mangu alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (Sarpcco) unaoendelea Arusha.
“Askari anapokuwa katika eneo la tukio anakuwa na tabia fulani ambayo kila mmoja wetu anayo kulazimisha mambo, ninyi ni wadau wetu lazima tufanye kazi pamoja hatuna ugomvi wowote na waandishi.
“Yanapotokea matukio ya aina hiyo ya kukamatwa au kusumbuliwa tujulishane kwa sababu askari wadogo wakati mwingine hufanya vitu ambavyo siyo msimamo wetu sisi viongozi wao,” alisema IGP Mangu.
Mangu pia alizungumzia matukio ya mauaji yanayoendelea wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani akisema ni uhalifu kama ulivyo mwingine wa kawaida na usitafsiriwe vinginevyo kwa sababu tayari umeanza kudhibitiwa.
Wakati IGP Mangu akisema hivyo, vyombo vya usalama vinawashikilia watu zaidi ya 60 katika mahabusu ya gereza la Kisongo kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi ikiwamo kurusha bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Massauni alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Sadc kuhakikisha uhalifu wa kuvuka mipaka unadhibitiwa.
Naye Katibu Mtendaji wa Sadc, Stegomena Tax, aliwahakikishia wakuu hao wa polisi kuwa Jumuiya anayoingoza itaendelea kutoa misaada na ushirikiano kila unapohitajika kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini