Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Lissu Awasha Moto

CHAMA cha Mawakili Tanganyika (TLS)   kimetangaza maazimio sita ikiwamo kufungua kesi ya  katiba Mahakama Kuu  kuhoji uhalali  wa Rais Dk. John Magufuli  kushindwa hadi sasa, kuteua Jaji Mkuu wa Tanzania.
  TLS pia imeazimia kumburuza mahakamani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kitendo chake cha kuvamia na kutenda makosa ya jinai katika Studio za Clouds Media Group  Machi 18, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari    mjini hapa jana, Rais wa TLS, Tundu Lissu, alisema   Baraza la Uongozi la chama hicho cha mawakili lililokutana kwa siku mbili mjini Dodoma, limetoka   na maazimio hayo muhimu kwa masilahi ya Taifa.

Alisema hatua ya kufunguliwa kwa kesi hiyo ya  katiba itasaidia kuhoji uhalali wa mkuu huyo wa nchi kushindwa hadi sasa kumteua Jaji Mkuu wa Tanzania.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), aliwahi kuibua mjadala mzito wa kuhoji uhalali wa   kuwa na kaimu Jaji Mkuu hadi sasa, jambo ambalo alidai linaitia doa taaluma ya sheria nchini.
Akifafanua kuhusu maazimio ya kikao hicho, Rais huyo wa TLS alisema tangu Jaji Mkuu Mohammed Chande, alipostaafu Januari Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli hajateua Jaji Mkuu mpya.
Alisema badala yake amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu.
Alisema Mahakama ya Tanzania  kama mhimili mkuu wa tatu wa dola kukosa kiongozi wake mkuu kwa takriban miezi mitano baada ya kustaafu kwa Jaji Chande kunatoa taswira kwamba Mahakama ina hadhi hafifu au ya chini ikilinganisha na Bunge na Serikali. 

“Dhana hii potofu inaathiri moja kwa moja heshima, hadhi na uhuru wa Mahakama ya Tanzania na haiwezi kuruhusiwa kujengeka miongoni mwa jamii yetu au Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hatoshelezi nafasi hiyo au miongoni mwa Majaji wa Rufaa au wa mahakama kuu hakuna hata mmoja mwenye sifa au uwezo wa kuwa Jaji mkuu.
“Ijapokuwa ibara ya 118(4) ya Katiba yetu inamruhusu Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu iwapo itatokea kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi au Jaji Mkuu hayupo au Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote lakini tunashangaa mtu kukaimu nafasi hiyo mpaka leo.
“Haijawahi kutokea katika historia yetu yote tangu uhuru Rais wa nchi yetu akashindwa kuteua Jaji Mkuu kamili kujaza nafasi iliyoachwa wazi ya Jaji Mkuu,’’ alisema  Lissu.
Alipoulizwa ni lini wanatarajia kwenda mahakamani, alisema haitachukua muda mrefu kuanzia sasa ingawa hatua ya awali itakapokamilika litaundwa  jopo la mawakili ambao watashughulikia suala hilo kwa utaalamu.

“Hapa lazima TLS iteue jopo la mawakili ambao watalipeleka suala hili mahakamani kitaalamu  kwa sababu  hapa kuna jinsi ya kuandika hati ya mashtaka  ambalo ni suala la utaalamu ambalo litachukua kama wiki mbili au tatu,’’ alisema Lissu.
MAJAJI WAKUU WALIOTANGULIA
Alisema kwa sasa nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania inakaimiwa na Profesa Ibrahim Juma, baada ya kuwa wazi kutokana na kustaafu kwa Jaji Mohammed Chande.
Majaji waliowahi kushika wadhifa huo na miaka yao katika mabano ni Philip Georges (1965-1971), Augustine Said (1971-1977), Francis Nyalali (1977-2000), Barnabas Samatta (2000-2007),  Augustino Ramadhan (2007-2010).
RC DAR KIKAANGONI
Rais huyo wa TLS, alisema baraza hilo pia limeazimia kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  kwa kumhusisha na tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai ikiwamo kutumia vyeti feki, ujambazi wa kutumia silaha na matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema watamfungulia mashtaka binafsi ya jinai kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai ikiwamo kutumia vyeti feki, ujambazi wa kutumia silaha na matumizi mabaya ya madaraka.
Lissu alisema dhana ya utawala wa sheria maana yake ni pamoja na mambo yote na  hakuna mtu aliye juu ya sheria  bila kujali cheo, nasaba au hali yake ya uchumi na yupo chini ya udhibiti wa sheria za kawaida za nchi na chini ya Mamlaka ya Mahakama za kawaida zilizoanishwa kwa mujibu wa Katiba.
“Kuna kifungu cha 120 cha kanuni za adhabu sura ya 16 ya Sheria za Tanzania kipo wazi kwa kutumia majina ya mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma hilo ni kosa pia ameathiri imani ya wananachi kwa serikali yao,’’ alisema.
Rais huyo wa TLS alisema azimio jingine waliloazimia ni kuandaa kongamano la  taifa juu ya mchakato wa Katiba Mpya ili kujadiliwa upya.
“Katiba mpya siyo matakwa ya mtu binafsi bali ni mchakato wa watanzania wote, mchakato wa katiba umekwama ni kwa nini umekwama Chama cha Mawakili hakiwezi kukaa kimya tutazungumza  hilo katika kongamano,’’alisema.
Lissu alisema haiwezekani Serikali itumie zaidi ya Sh bilioni 121 katika mchakato wa kura za maoni halafu wao wakiwa wanasheria   wakae kimya.
MAKATO KWA WAFANYAKAZI
Alisema asilimia 50 ya mshahara wa mfanyakazi unakatwa kodi hali ambayo imekuwa ikichangia wafanyakazi wengi kuishi maisha ya taabu na shida kubwa kwa vile fedha nyingi hukatwa katika kodi mbalimbali.
“Unakuta mpaka ufikishe miaka 60 ndiyo unatakiwa upewe kiinua mgongo chako… nani atafikisha huko jamani?
“Wengi wanaumizwa na kunyang’anywa haki zao eti ukiachishwa ajira hupati kitu, nani kasema hali ya maisha na maradhi nani atafikia huko,TLS hii itakuwa ni agenda yetu,’’alisema.
Pia alisema azimio jingine ni  suala la mafao ya kujitoa uanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Alisema wameazimia  kulishughulikia suala hilo kwa kina kutokana na wafanyakazi kuathirika nalo.
Lissu alisema azimio jingine   ni kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji Tanzania kwa kuhakikisha haki inapatikana pande zote.
AWAITA WALIOFUKUZWA
  Lissu pia amewataka wafanyakazi 9,932  waliopatikana kuwa na vyeti feki, kutulia na kama wameonewa waende katika Chama hicho kwa ajili ya kusaidiwa ushauri wa  sheria.
“Si wametangaza juzi tu, hatujui lakini wapo kweli wenye vyeti feki lakini kuna wengine wameonewa.
“Tunasubiri wajitokeze, tutawasaidia maana katika Serikali hii huwezi kusema watakosekana walioonewa,’’alisema.
KUGUSWA WANASIASA
Kuhusu kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,  Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki kuwa uhakiki wa watumishi hewa hautawagusa wakuu wa mikoa, wilaya na wanasiasa, Lissu alisema inatokana na Serikali kuhofia kelele za wanasiasa.
“Haya ni maoni yangu binafsi siyo kama Rais wa TLS. Wangeguswa wanasiasa kelele zingekuwa nyingi maana tunajua Serikali hii ni kubebana bebana tu,’’ alisema.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017