Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Lwandamina Atoa Onyo Kali Kuhusu Ubingwa Yanga SC

George Lwandamina
KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, amesema mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City ulikuwa mgumu zaidi kwao kutokana na presha ya kuusaka ubingwa huku wapinzani wao wakicheza vizuri zaidi yao, lakini walitulia na kutumia vema nafasi mbili walizozipata.

Akizungumza  muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Lwandamina alisema kwa sasa haoni kizuizi cha kutwaa ubingwa msimu huu, lakini akaonya wachezaji wasibweteke katika mechi mbili zilizobaki.

"Ushindi huu sasa unatupa uhakika wa kutetea ubingwa wetu, haikuwa safari nyepesi kufika hapa, nawashukuru sana wachezaji wangu kwa kazi nzuri wanayoifanya," alisema Lwandamina.

Aidha, alisema pamoja na kupata ushindi kwenye mchezo huo, anaamini bado hawajamaliza kazi na wanapaswa kuwa makini katika michezo yao yote miwili iliyobakia.

"Mpira ni mchezo wa maajabu sana, huwezi kujiaminisha kuwa kazi imekwisha, tuna michezo miwili na tunapaswa kushinda yote," alisema Lwandamina.

Ushindi huo wa juzi umeiweka Yanga karibu kabisa na ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuishusha Simba kileleni lakini kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kutokana na timu zote kuwa na pointi 65, lakini kikosi cha Lwandamina kikiwa na mechi mbili mkononi cha Joseph Omog mechi moja.


Msuva kuikosa Toto Africans

Katika hatua nyingine, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo Simon Msuva hatoweza kucheza mchezo wa kesho dhidi ya Toto Africans.
Msuva aliumia kwenye mchezo wa juzi na kushonwa nyuzi sita.


"Nimeongea naye anasema kidogo ana nafuu japo bado anasikia maumivu..., hatocheza mchezo wa Jumanne (kesho) labda mechi ya mwisho dhidi ya Mbao FC," alisema Hafidhi

Msuva ndiye anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji akiwa na mabao 14.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017