Makali ya uhakiki wa vyeti feki, yameacha vilio, maumivu na mateso, kufuatia agizo la kuwaondoa na kuwafuta kazi pamoja na kukatwa kwa mishahara kwa watumishi wa umma wapatao 9,932 kwa kosa la kughushi vyeti ambapo uchunguzi wa gazeti hili umebaini dalili za kuwepo kwa majanga 10 kufuatia sakata hilo, twende aya kwa aya.
Katika chimbuachimbua yetu siku chache baada ya uamuzi huo uliotolewa na Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ mjini Dodoma katika sherehe ya miaka 10 ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), limeibuka na taarifa zinazoonesha madhara mengi zaidi, lakini yenye ujazo mkubwa wa tani na kilo ni haya hapa chini.
Uamuzi huo ulitolewa na Rais Dk. Magufuli, zikiwa zimebaki siku nne kabla ya mishahara kuanza kusoma kwenye miamala, watumishi hao wakiwa na matarajio ya kuchukua ‘mitonyo’ yao ambayo kwa kawaida ilikuwa kwenye mipango mingi, hivyo kuondolewa kazini ghafla na kutopewa mshahara wa Aprili, kumewashtua na kuwaathiri kisaikolojia kwani imeonesha wengi hawakuwa na pesa zaidi ya kutegemea mishahara.
VILIO TAASISI ZA FEDHA, VIKUNDI VYA MIKOPO
Janga lingine ambalo limeibuliwa na uchunguzi wa Uwazi ni lile la baadhi ya watumishi hao kuwa na mikopo kibao kwenye taasisi za fedha yakiwemo mabenki na zile benki ndogondogo za vijijini (village cooperative banks, Vicoba), hivyo kitendo cha watumishi hao kuondolewa kazini na kukatwa kwa mishahara kumesababisha kushindwa kurejesha mikopo hiyo na kuleta vilio na mtikisiko kwa taasisi husika.
Miongoni mwa walioachishwa kazi, wamo waliokuwa wakitegemea mishahara kusomesha watoto kwenye shule za kulipia hivyo sakata hilo limewafanya baadhi yao kusitisha huduma hiyo na kuwaondoa watoto wao kwenye shule hizo.
TATIZO LA MAKAZI
Uchunguzi ambao haukumtoa jasho la ubongo mwandishi wetu, ni ule wa athari za makazi, kwamba wengi au baadhi ya watumishi hao wanaishi kwenye nyumba za kulipia (za kupanga), jambo lililo wazi ni kwamba kuna waliotakiwa kulipa pango la nyumba mwishoni mwa mwezi Aprili, wengine mwezi mmoja au miwili ijayo, hivyo vurumai hii imezua janga la makazi yao na familia kwa ujumla.
Kwa vyovyote vile, wote waliotumbuliwa kwa vyeti feki lazima wapambane kumudu maisha kabla ya kusimama na kuendelea na shughuli zingine. Hatari inayoonekana kuwepo kwa siku za hivi karibuni, waliokuwa watumishi hao kuanza kuomba misaada ‘kupiga mizinga’, kwa watu wa karibu ili kujinusuru na ugumu wa kutokuwa na kazi.
Tumetumia jicho la tatu kuchungulia nyuma ya ukuta, ambapo kumebainika harufu ya mitafaruku mingi ya kindoa kwa baadhi ya wahusika kutokana na kusitishwa kwa huduma muhimu, ikiwemo ya fedha jambo ambalo linaweza kusababisha hata kuvunjika kwa baadhi ya ndoa.
Hata hivyo, zipo duru zilizobaini kurejea kwa nidhamu kwenye ndoa kwa wale waliokuwa na michepuko kwa vile jeuri ya kumiliki wapenzi zaidi ya mmoja imeondoka, hivyo kurejesha ‘majeshi’ nyumbani.
Kuna waliokuwa na mipango ya maendeleo ikiwemo umaliziaji wa ujenzi wa nyumba, ofisi na miundombinu mingine, lakini sasa kila kitu kimetibuka kama si kudoda kwani wahusika wanalazimika kujipanga upya.
Mdororo wa kiuchumi miongoni mwa watumishi hao, utasababisha matatizo mengi. Wengi watashindwa kutumia usafiri binafsi kwa maana ya magari sababu zikiwa ni kushindwa kumudu gharama za mafuta na matengenezo, hivyo kupaki magari yao majumbani.
TAMKO LA RAIS
Mara baada ya kukabidhiwa ripoti ya watumishi walioghushi vyeti na kuajiriwa na serikali Ijumaa iliyopita, Rais Magufuli aliwataja watumishi hao kuwa ni sawa na wezi na majambazi, hivyo wajiondoe kabla ya Mei 15, mwaka huu, kabla hawajafikishwa mahakamani ambapo wanaweza kupewa vifungo hadi miaka saba jela kwa wale watakaokutwa na hatia, kama sheria zinavyosema.
Rais aliagiza pia watumishi hao wasilipwe mishahara na nafasi zao za kazi zitangazwe ili weye sifa waombe na kuajiriwa ili wazizibe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki aliyekabidhi ripoti ya wenye vyeti feki kwa rais alisema imebainika pia watumishi 1,538 wamekuwa wakitumia vyeti vinavyofanana huku 11,596.
KUTOKA MEZANI KWA MHARIRI
Maisha si lazima yaende mbele kwa kazi za kuajiriwa. Ardhi yetu ina rutuba bora istawishayo mazao ya biashara na chakula, ingawa ni vigumu kuanza upya lakini hakuna budi.
Hivyo, kwa wote waliokumbwa na sakata la vyeti feki, ni wakati wa kujipanga upya kwa kushiriki kazi za kilimo (kama wanaweza) au nyingine zozote za kujiajiri wenyewe na maisha yasonge lakini wakiwa na somo kubwa kwa siku za mbele juu ya utumishi wao ili iwe msaada kwa watoto wao na watu wengine wasikumbwe na uhakiki-Mhariri.
SOMA ORODHA YOTE HAPA
-Credit:GPL
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini