NJOMBE: Mabinti pacha walioungana kiwiliwili ambao ni yatima, Consolata na Maria Mwakikuti (19) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoa mpya wa Njombe, waliofanya mitihani ya kidato cha sita mwaka huu na kumaliza leo (Jumanne) wameeleza ndoto zao kimaisha baada ya masomo.
KAZI WANAYOIPENDA
Wakihojiwa na mwandishi wetu wiki iliyopita wasichana hao walisema wanapenda kazi ya ualimu pindi watakapohitimu chuo.
“Tunapenda kuwa walimu kwa sababu hiyo ni kazi ya wito ili tumtumikie Mungu,” alisema Consolata.
MUME WAMPENDAYE
Walipoulizwa wangependa kuolewa na mwanaume wa aina gani, Consolata alisema baada ya kumaliza masomo yao ya chuo wangependa kuolewa na mwanaume mcha Mungu, mwenye upendo wa dhati na ambaye anajiheshimu na wao watamheshimu.
“Awe na tabia nzuri na mcha Mungu, mwanaume huyo anaweza kufikiri kuwa tutakuwa mzigo kwake lakini, hapana tutapigana katika maisha na tutamheshimu,” alisema Consolata.
“Tungependa nasi tuwe na watoto,” alisema Maria pacha mwingine.
Baadaye mapacha hao, walimuonesha mwandishi wetu walivyo mahiri kwa kuimba nyimbo za Injili.
ELIMU YA MSINGI
Itakumbukwa kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema walitaka kuwa wasomi waliobobea katika utaalam wa kompyuta na ukatibu muhtasi lakini sasa wanapenda kuwa walimu.
ILIKUWA WASOME JANGWANI DAR
Pacha hao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es Salaam hata hivyo wakaenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Pacha hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
“Wala hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia,” alisema Consolata anayeonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Pacha hao walizaliwa wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete, mkoani Iringa mwaka 1996.
Walifaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010. Katika mtihani wa kidato cha nne kila mmoja alikuwa na namba yake ya mtihani (Maria-S. 283/0004 na Consolata S 283/0009) na walifaulu vizuri ndipo walichaguliwa kujiunga na kidato cha sita.
Pacha hao wanalelewa na mama yao mlezi Betina Mbilinyi akisaidiwa na Magdalena Mbilinyi kwenye Kituo cha Nyota ya Asubuhi, Kilolo.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini