Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Walimu Watupwa Jela Miaka 20 Kwa Wizi Wa Mitihani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu imewahukumu walimu wawili wa shule ya sekondari Nyawa na Shishani  zilizopo Wilaya ya Bariadi na Itilima mkoani hapa kwenda jela miaka 20 kila mmoja kwa kosa la kuiba na kuvujisha mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
Walimu hao waliohukumiwa ni Issa Makene (40) wa Sekondari ya Shishani pamoja na Solela Mangura (26) mwalimu wa kujitolea shule ya sekondari Nyawa ambaye hakuwepo mahakamani wakati hukumu hiyo ikitolewa.
Awali akiwasomea shitaka linalowakabili walimu hao katika kesi namba 176/2015, kabla ya hukumu kutolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, John Nkwabi, mwendesha mashitaka wa serikali, Mosses Mafuru alisema tukio hilo lilitokea Novemba 10, mwaka 2013, katika shule ya Sekondari Sagata.
Mafuru alieleza kuwa Mwalimu Makene akiwa mkuu wa kituo cha kufanyia mtihani huo katika Shule ya Sekondari Sagata baada ya kupangiwa, siku ya tukio wakati wa chakula cha jioni aliwalaghai askari waliokuwa wakilinda mtihani katika kituo hicho.
Alisema kuwa Makene aliwaomba askari hao kumpatia ufunguo wa chumba kilichokuwa kimehifadhi mitihani hiyo kwenye kabati ambalo mitihani hiyo ilikua imehifadhiwa.
Mafuru aliendelea kuielezea mahakama kuwa mara baada ya kufungua kabati hilo mtuhumiwa alichukua bahasha ya mtihani wa somo la fizikia wa kuandika (paper one theory) kisha kwenda kuuficha chini ya uvungu wa kitanda chake shuleni hapo.
Alieleza kuwa kesho yake baada ya mwalimu huyo kuchukua bahasha hiyo Novemba 11, 2013 mtuhumiwa alichana bahasha kisha kutoa karatasi moja ya mtihani huo na kumkabidhi mwalimu mwenzake wa kujitolea Solela.
Alisema walimu hao walikuwa kwenye harakati za kuwapatia wanafunzi 15 wa shule hiyo ambao mwendesha mashtaka huyo aliwataja majina yao kuwa ni Abasi Makwaya, Veronica Jonathan, Mboji Masike, Saka Masuki, Milembe Mabula, Makula Saya na Prisca Jonathan.
Wengine ni Getruda Senga, Buye Masike, Msafiri Samson, Japhet Martine, Alex Jackson, pamoja na Khamis Nkwabi.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo Hakimu John Nkwabi aliwahukumu washitakiwa hao kwenda Jela miaka 20 kila mmoja, kwa maelezo kuwa mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Akizungumzia hukumu hiyo Ofisa Elimu wa Mkoa, Julias Nestory alisema haki imetendeka na imekuwa fundisho kwa walimu wengine.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017