WALIMU mkoani hapa wametakiwa kushirikiana na wazazi katika kuwafundisha wanafunzi matumizi mazuri ya mitandao hususan simu za mikononi katika mazingira yasiyoharibu maadili yao.
Akizungumza katika mahafali ya kuhitimu darasa la saba katika shule ya Msingi Airport hivi karibuni, Katibu wa Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, Abdulikadri Mushi, alisema kuwa kwa sasa Dunia iko katika kipindi cha utandawazi na watoto wadogo wako msitari wa mbele kuharibiwa na utandawazi huo, kwani hutaka na wao kwenda na wakati.
Alisema kuwa, sasa hivi watoto wadogo wanajua kutumia mitandao hasa simu za mikononi na kompyuta na wengi hutumia kwa matumizi mabaya, ambayo husababisha kujifunza na kuiga mambo mabaya.
“Utakuta watoto wanaangalia picha chafu kwenye simu zao, pia hata kwenye kompyuta, kwani picha hizo zinapatikana kwenye mtandao,” alisema Mushi.
Sambamba na hayo, Mushi aliahidi kujenga jengo la choo ili kupunguza kero ya wanafunzi ya kuhangaika baada ya kilichokuwepo awali shule hiyo kubomoka.
Naye Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Katubuka, Tatu Rajabu (CHADEMA), alisema jukumu la kuhakikisha mtoto anakuwa katika mazingira mazuri yenye maadili ni la mzazi pia walimu.
“Mzazi huachana na mtoto asubuhi na mtoto hushinda na walimu kwa muda mwingi, hivyo walimu wawe na mzigo katika kuwafundisha na kuwaonya watoto katika mambo ambayo hupelekea kuharibika kwa maadili,” alisema Rajabu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wanajeshi Wastaafu, Nicas Bukobero, alisema kuwa kazi ya walimu ni kuwafundisha na kuwalea wanafunzi katika maadili mema na sio kuwaacha waharibiwe na utandawazi.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini