Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na uvumi unaosambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, juu ya kuwepo kwa mchele wa plastiki, unaodaiwa kuingizwa nchini na wafanyabiashara wasio waaminifu, unaouzwa katika vibanda vya akina mama n’tilie.
Baada ya uvumi huo kuleta hofu kubwa kwa wananchi, hasa kufuatia video mitandaoni kuonyesha wali uliopikwa ukiliwa na hata kiwanda kinachodaiwa kuwepo nchini kinachotengeneza mchele huo, Risasi Jumamosi liliamua kuufanyia kazi uvumi huo ili kujua mbivu na mbichi ya sakata hilo.
Risasi Jumamosi liliambiwa kuwa mchele huo unauzwa katika baadhi ya masoko ya jijini Dar es Salaam yakitajwa kuwa ni pamoja na yale ya Buguruni, Mwananyamala, Makumbusho na Afrikasana.
Kikosi kazi kilisambazwa katika masoko hayo na kufanya uchunguzi wake ikiwa ni pamoja na kuzungumza na baadhi ya wanaouza bidhaa hiyo.
Lucas Kimadi wa Soko la Makumbusho anasema; “Hata hivyo, ingawa nimesikia juu ya tetesi hizo kiukweli sijawahi kuuona machoni mchele huo wa plastiki. Ila nimewahi kusikia siku za nyuma kuwa kuna wafanyabiashara walikuwa wanauingiza kinyemela na serikali iliwachukulia hatua.”
Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mwesigwa, alipoulizwa juu ya kuwepo kwa mchele huo, alisema anavyofahamu, hayo ni maneno ya mitandaoni, kwani hajawahi kuuona.
“Sasa kama ni wa plastiki utaupikaje na uwe tayari kwa kula. Watu wameamua kuvumisha tu lakini sidhani kama kuna ukweli katika hili, na ninakubaliana kabisa na TFDA pengine hiyo video ambayo tumeiona mtandaoni inaonesha namna ya kutengeneza mifuko.”
Hali kama hiyo ilikuwepo pia katika masoko yote ambako Risasi Jumamosi lilitembelea, kwani wafanyabiashara wote walionyesha kushangazwa kwao na madai hayo, wakisema hivi sasa baada ya mavuno, wanapata mchele mwingi kutoka Mikoa ya Mbeya, Rukwa, Morogoro na Mwanza na kwamba siyo rahisi kwao kuuza wala kununua mchele wa plastiki.
“Mimi kiukweli nimewahi kusikia hata hapahapa kwamba kuna watu walikuwa wanauuza mchele huo kinyemela, lakini sijawahi kuwaona kwa macho wala kuuona mchele wenyewe.
“Nahisi hayo ni maneno ya mitandaoni, nimekuwa nikisikia mara kwa mara watu wanasema juu ya hilo lakini sijawahi kabisa kupata mtu wa kunithibitishia kuwa mchele wenyewe huu hapa,” alisema Rajabu Simba wa Soko la Mwananyamala.
“Nimeona kwenye mitandao kuwa mchele huo upo lakini sijawahi kuuona, kununua wala kushawishiwa kuuziwa ili nije nifanye biashara.”
Naye katibu wa soko hilo, Furahisha Kambi alisema sokoni hapo hakujawahi kutokea tetesi za kuwepo kwa mchele wa plastiki ingawa amewahi kuzisikia mara kadhaa huko nyuma.
Wakati kikosi kazi hicho kikiwa kazini, mara zikaibuka taarifa za kiintelijensia, zikisema kuwa askari polisi walikuwa wakijiandaa kwenda kuvamia kiwanda kimoja huko Kiwalani Minazi Mirefu, kinachodhaniwa kuwa ndicho kinachozalisha mchele huo wa plastiki.
Mara moja, kikosi hicho kilijigawa na kufanikiwa kujiunga na wanausalama hao, ambao kwa wakati huo walikuwa wakiandaa hati maalum ya upekuzi (Search Warrant).
Msafara wa watu hao wa usalama uliwasili eneo la tukio wakiwa chini ya ofisa mmoja ambaye alikataa jina lake kuandikwa gazetini na kuikuta nyumba inayotumika kama kiwanda, mbele ikionyesha kuwa ni duka la unga, mchele kwa bei ya jumla.
Ndani ya kiwanda hicho, kilichokuwa na wafanyakazi wachache wa kiume na kike, Risasi Jumamosi lilishuhudia mashine zikiunguruma huku rola za plastiki zikizunguka na kuishia kwenye kitu kama ndoo ambapo punje za kitu kama mchele zilionekana kudondokea.
Risasi Jumamosi lilishuhudia punje hizo na kuzishika zikifanana kwa kiasi kikubwa na zile za mchele, lakini mmiliki wa kiwanda hicho, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mika, alisema kinachoonekana kama mchele, ni ‘matirio’ ya kutengeneza plastiki.
“Hapana mwandishi, huo siyo mchele, hayo ni matirio ya plastiki ambayo ndiyo tunatengenezea hii mifuko unayoiona.”
Alipoulizwa kwa nini nje ya kiwanda, kumeandikwa kama kunauzwa mchele na unga badala ya mifuko ya plastiki, alisema awali kiwanda hicho kilitumika kama duka la jumla la bidhaa hizo na yeye hakuwa amefuta tangazo hilo.
“Aaaa unajua hili jengo hapo awali lilikuwa likitumika kama mashine ya kusaga na kuuza huo unga na mchele, alivyohama mimi ndiyo nikalichukua na kuendeshea hii biashara yangu ya kuzalisha mifuko ya plasti.
Maofisa wa Polisi waliokuwemo katika msafara huo, baada ya kufanya naye mahojiano ya kina na kujiridhisha jinsi utengenezaji wa mifuko hiyo ya plastiki ulivyo, walimuachia mmiliki huyo.
Wakati tayari Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ikiwa imetoa tangazo la kupinga kuwepo kwa bidhaa hiyo sokoni, Risasi Jumamosi linaweza kuripoti kwa sasa kuwa uvumi juu ya kuwepo kwa mchele wa plastiki sokoni ni uongo, unaoenezwa na watu wenye malengo wanayojua wenyewe.
Hata hivyo, bado linaendelea kufuatilia kwa karibu tetesi hizo na litatoa taarifa nyingine haraka kwa wasomaji na vyombo vinavyohusika endapo litabaini kuwepo kwake, sambamba na wote wanaoeneza taarifa hizo zenye kuwatia hofu wananchi.
Yusuf Miraji wa Afrikasana alisema amefanya biashara hiyo kwa muda mrefu, lakini hajawahi kuuona mchele wa plastiki. Alidai huenda watu wanachanganya ule wa Basmati, wakidhani ndiyo wa plastiki.
Katika Soko la Buguruni, Risasi Jumamosi lilifanikiwa kuzungumza na Halima Msuye, muuzaji wa mchele wa muda mrefu katika soko hilo ambaye alisema;
TAZAMA VIDEO YA TUKIO ZIMA HAPA
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini