Benjamin Sawe-Maelezo
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imesaini mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha bandari utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa za mizigo na kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari ya hindi.
Upanuzi huo utakaofanywa na kampuni ya China Harbor Construction ya China utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36, ambapo utahusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari na uongezaji wa kina cha maji kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hatua hiyo inalenga kuifufua upya bandari ya Dar es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani na kuhudumia wateja wengi kuliko ilivyo sasa.
“ Kukamilika kwa upanuzi na uongezaji wa kina cha maji katika gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8 hadi 15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba hadi makontena elfu kumi na tisa kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa Tanzania”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa pamoja na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge toka Dare s Salaam hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari ya Dar e s Salaam kufanya kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi hivyo nawataka wafanyakazi wote wa bandari kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko amesema kiasi cha dola za Marekani milioni 421, kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo ambapo kati ya fedha hizo Benki ya Dunia itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa adha ya baadhi ya meli kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya bandari ya Dar es salaam na kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini