Katika ripoti ya pili ya Kamati ya kutathmini mchanga wa madini Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge ametajwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa alikuwa na mchango mkubwa wa kulisababishia Taifa hasara kubwa kutokana na kuandaa au kusaini mkataba mbovu wa madini unaoyaruhusu makampuni ya uchimbani kusafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi pamoja na kukubali viwango vidogo vya mrabaha kwa Taifa katika sekta ya madini.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa kwa Rais na Mwenyekiti wa kamati hiyo ni pamoja na kuwashughulikia viongozi na watendaji wote wa Serikali walioshiriki kusababisha hasara hii kwa zaidi ya miaka 19.
Rais Dkt. Magufuli akiongelea pendekezo hili aliagiza vyombo vinavyohusika viwaite watu wote waliotajwa ili wahojiwe.
Baada ya kauli hiyo ya Rais, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa Chenge ataendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge mpaka atakapoitwa na kuhojiwa kuhusu mchanga wa madini (makinikia). Spika Ndugai alisema hakuna kanuni inayomzuia Chenge kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bunge kwa sasa.
“Kwa sasa hapana. Ataachia nafasi hiyo atakapoitwa kuhojiwa; akishathibitika ndio atatoka kwenye nafasi ya Uenyekiti,” alisema.
Utaratibu unaeleza kwamba Ofisi ya Spika ikishapata taarifa ya Mbunge au kiongozi fulani wa Bunge kuhitajiwa na chombo cha dola na Spika akatoa ruhusa hiyo, Mbunge huyo ataachia madaraka yake na kubaki na ubunge tu.
Mwenyekiti wa kamati ya pili ya kuchunguza hasara iliyoletwa na kusafirisha mchanga wa madini, Profesa Nehemiah Osoro alisema kuwa wakati Taifa linapitisha Sheria na mikataba ya hovyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Andrew Chenge.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini