Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Bingwa Ligi Kuu Tanzania Bara Kupatikana Hivi, Tofauti Kabisa Na Msimu Uliopita.


Mpaka sasa Simba imefunga mabao mengi kuliko magoli yote yaliyofungwa na Yanga na Azam baada ya kuchezwa kwa michezi tisa ya Ligi Kuu Bara.

Aidha kasi ya ufungaji wa mabao kwa Yanga na Azam imezidi kuporomoka ukilinganisha na msimu miwili iliyopita wakati Simba wakipanda baada ya kuchezwa kwa mechi tisa za Ligi Kuu.

Simba ndio kinara ikiwa imefunga mabao 21 na kuruhusu matano wakati Yanga ikiwa imeshafunga mabao 11 na kuruhusu manne wakati Azam imepachika mabao saba na kuruhusu mawili.

Jambo la kutia moyo kwa timu hizo tatu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu ni kuimarika kwa safu ya ulinzi katika kipindi cha misimu mitatu mfululizo.

Hali hiyo inaonyesha kuleta wasiwasi kuwa msimu huu hadi kufikia mwisho wa msimu kunaweza kukawa na idadi ndogo ya mabao kwa timu hizo tatu ukilinganisha na misimu miwili iliyopita.

Katika msimu wa 2015 /2016 hadi kufikia mechi za raundi ya tisa ya ligi, Yanga ilikuwa imefunga mabao 22 wakati Azam ilifunga mabao 20 Simba ikifunga mabao 15, lakini ajabu timu zote tatu ziliruhuu mabao matano kila mmoja.

Katika msimu huo hadi mwishoni mwa ligi ambao Yanga ndio waliibuka mabingwa walikuwa wametikisa nyavu za wapinzani mara 70, na kuruhusu mabao 20 wakati Azam ilifunga mabao 47 na kuruhusu 24 huku Simba ikifunga mabao 45 na kuruhusu 17.

Msimu uliopita hadi kufikia mechi za raundi ya tisa mabingwa watetezi Yanga walikuwa wamepachika wavuni mabao 14 na kuruhusu matatu, wakati Simba ilifunga 16 na kuruhusu matatu huku Azam ikifunga 10 na kuruhusu manane.

Katika msimu huo hadi mwisho wa msimu mabingwa Yanga walifunga mabao 57 na kuruhusu 14, Simba ilifunga mabao 49 na kuruhusu 17 wakati Azam ilifunga mabao 36 na kuruhusu 20.

Hali hiyo inaonyesha kuwa Simba imeimarika katika ufungaji wa mabao na inabebwa na usajili iliofanya msimu huu kwa kuwaongeza Emmanuel Okwi na John Bocco ambao wanasaidia na Shiza Kichuya na Laudit Mavugo.

Okwi ndiye kinara wa ufungaji akiwa amefunga mabao manane akifutiwa na Kichuya aliyefunga matano, Mavugo, Mzamiru Yassin wamefunga mawili kila mmoja wakati Bocco na Juma Liuzio na Erasto Nyoni wakifunga moja kila mmoja.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Simba ukiangalia wamebeba na ushindi wa mabao mengi katika mechi ya kwanza kauli iliyoungwa mkono na Sekilojo Chambua.

“Uwepo wa Okwi umekuwa chachu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwani licha ya kwamba mabao yake yote kafunga uwanja wa Uhuru, lakini ni mchezaji mwenye kiwango na kaichangamsha safu ya mbele ya Simba,” alisema Mayay.

Zamoyoni Mogella alisema kurejea kwa Okwi kumeichangamsha safu ya ushambuliaji ya Simba msimu huu ingawa ni mapema mno kuitabiria makubwa kwa wachezaji wengi wa Ligi Kuu ni kama wana homa ya vipindi.

"Wameanza vizuri na ujio wa Okwi umeifanya safu ya ushambuliaji ya Simba kuwa hatari ingawa bado wanatakiwa kuongeza nguvu kama kweli wanautaka ubingwa"alisema Mogella

Yanga inabebwa mshambuliaji, Ibrahim Ajib mwenye mabao matano, inaathiriwa zaidi na kukosekana kwa washambuliaji wake muhimu kama Simon Msuva aliyehamia Difaa El Jadida ya Morocco pamoja na Amissi Tambwe na Donald Ngoma walio majeruhi muda mrefu.

Ngoma ameshaifungia timu hiyo mabao mawili, wakati Obrey Chirwa akifunga mabao matatu huku kiungo Pius Buswita akiwa amefunga bao moja.

Beki wa zamani wa Yanga, Mayay alisema Yanga inaathiriwa na kuondoka kwa Msuva huku pia majeruhi ya Tambwe nayo yakichangia kutokuwa vizuri katika ufungaji msimu huu.

"Ukiangalia misimu mwili iliyopita Yanga waliongoza si kufunga mabao tu hata kutengeneza nafasi nyingi na yote ilichangia kuwepo kwa Msuva na kina Tambwe ambao walikuwa katika ubora wao.

“Msuva hayupo na Tambwe ni majeruhi muda mrefu wakati Ngoma naye licha ya kucheza mechi kadhaa, lakini hajafikia hata asilimia 50 ya ubora wake wa msimu uliopita,” alisema Mayay.

Naye Chambua alisema Yanga ina tatizo kubwa katika umaliziaji kwani hivi sasa wanamtegemea Ajib pekee kwa kuwa washambuliaji wengine ni majeruhi na wengine hawapo katika kiwango.

"Ukimuondoa Ajib, Yanga inaaangushwa na washambuliaji kwani ukiangalia Chirwa ana kiwango kizuri lakini hayupo vizuri kweny kufunga. Ngoma naye bado anasuasua hajaonyesha thamani yake hivyo akirejea kutoka kwenye majeruhi napaswa kubadilika ili kuisaida timu lakini pia kukosekana kwa Tambwe ambaye ni mfungaji wa mabao mengi ya Yanga kunaigharimu timu hiyo."

Azam anayeongoza kwa kufunga ni Mbaraka Yusuph mwenye mabao matatu akifuatiwa na Yahya Zayd, Himid Mao, Yahaya Mohammed na Paul Peter mwenye bao moja kila mmoja.

“Azam kilichowagharimu ni kubadilisha badilisha wachezaji kwani tangu aondoke Kipre Tchetche ambaye alikuwa mfungaji wao mahiri na sasa Bocco wamekuwa wanaleta wachezaji tofauti katika nafasi hiyo jambo ambalo bado halijawaletea manufaa," alisema Mayay.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017