Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupitia mkutano mkuu wa 16 wa wanachama uliofanyika jijini Dar es Salaam, kimeweka maazimio manne kufuatia hoja zilizoibuliwa baada ya mjadala wa hali ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika nchini ambayo ilikuwa dhima kuu ya mkutano huo.
Kabla ya kuweka maazimio hayo, wanachama walijadilia kuhusu hali ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika mbali na wadau mbalimbali kupaza sauti, ambazo zimedaiwa kueendelea kuwa mbaya nchini Tanzania.
Taarifa iliyotolewa leo (Jumamosi) na LHRC imeeleza kuwa vya vyama vya siasa na wananchi kuzuiwa bila sababu za msingi vimeendelea kushamiri huku uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mtu mmoja mmoja kueleza hisia zake ukiendelea kuwa shakani.
Kutokana na hilo wanachama wameazimia kutumia vyombo vya kikanda na kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na mahakama za kikanda na kimataifa ili kutolea ufafanuzi na kusaidia kwa nafasi yao utatuzi wa hali ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa demokrasia nchini.
Wanachama pia wameazimia kuongeza nguvu katika kufungua kesi mkakati ili kuboresha sheria zinazokinzana na haki za binadamu na hatimaye kupata katiba bora.
Azimio lingine ni kuendelea kuyajengea uwezo makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa Serikali, wabunge, mahakama, jeshi la polisi, viongozi wa dini pamoja na wananchi juu ya umuhimu wa kuheshimu na kulinda haki za binadamu katika kufanikisha maendeleo ya nchi.
Kudumisha ushirikiano na mshikamano baina ya asasi za kiraia na wadau mbalimbali wa haki za Binadamu ikiwemo vyombo vya habari katika kuifikia Jamii yenye Haki na Usawa.
Mkutano huu wa 16 ulitawaliwa na dhima inayosema, ‘Hakuna Maendeleo bila Uhuru wa Kujieleza na Uhuru wa Kukusanyika.’
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini