MKAZI wa kijiji cha Tunyi, kata ya Mambwe- Nkoswe, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa, Matipa Sizunzu (20), aliyedaiwa kuuawa kwa kuliwa na fisi zaidi ya miezi 10 iliyopita, ameonekana akichunga mifugo ya mmoja wa wafugaji kijijini humo aitwae Juma Maeka.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza pia, mfugaji huyo amekataa kumrejesha kijana huyo kwao hadi hapo ndugu zake (Sizunzu) watakapomlipa Sh milioni moja alizowapatia kama ubani wakati walipofanya msiba wa kijana huyo. Sizunzu alipotea katika mazingira ya kutatanisha Septemba mwaka jana na ndugu zake baada ya kumtafuta bila mafanikio, waliweka msiba wakiamini kuwa amekufa. Kuonekana kwa kijana huyo kijijini humo akichunga mifugo huku wanakijiji wakijua kuwa alikufa, kumezua taharuki kubwa kijijni humo.
Taarifa kutoka kijijini humo zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa mfugaji huyo, Maeka aligoma kumrejesha kijana huyo kwa ndugu zake akiwataka ndugu hao wamlipe kiasi hicho cha fedha Sh milioni moja. Diwani wa kata hiyo, Julius Siwale, alisema kabla ya kupotea kwa kijana huyo alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe wa mfugaji huyo , ambaye wakati wa msiba wake aliwapatia wafiwa ubani wa Sh 1,000,000. “Baada ya msiba kumalizika kila mtu kijijini hapa aliamini kuwa kijana huyo alikuwa amefariki dunia lakini sasa hatuamini macho yetu baada ya ndugu wa kijana huyo kumkuta akichunga ng’ombe za mfugaji huyo (Maeka ) mbugani kijijini humo,” alieleza .
Alisema kuwa ndugu wa kijana huyo walitaka aongozane nae hadi nyumbani kwako kijijini humo, lakini mfugaji huyo alikataa akidai hadi alipwe fedha zake alizotoa kwa wafiwa kama ubani. Diwani alisema kuwa baada ya malumbano yaliyodumu kwa muda mrefu baada ya ndugu wa kijana huyo na mfugaji huyo, uongozi wa kata hiyo ulilazimika kuingilia kati kwa kuitisha kikao cha dharura ambapo walimwamuru mfugaji huyo kumrejesha mara moja kijana huyo kwao. Alisema kuwa katika kikao hicho mfugaji huyo aliamriwa kulipa Sh 100,000 ikiwa ni fidia kwa ndugu wa kijana huyo.
Naye Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Oswald Kalindo, alisema awali kila mtu alikuwa akijua kuwa kijana huyo alikuwa amekufa kwani walitafuta kila kona ya kijiji na maeneo mengine kwa muda mrefu bila mafanikio hatimaye wana ndugu wakaamua kuweka msiba wakiamini kijana huyo ameuawa na kuliwa na fisi. Alisema kupatikana kwa kijana huyo kumeleta faraja kwa wakazi wa kata hiyo kutokana na kwamba kila mmoja alikuwa na wasiwasi juu ya kupotea kwake katika mazingira ya kutatanisha.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini