SIKU chache baada ya kuwekwa hadharani majina ya watumishi walioghushi vyeti na wenye malalamiko kuanza kumiminika katika ofisi za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), kutaka ufafanuzi wa uhakiki wa taarifa zao, baraza hilo limewataka watumishi hao kupeleka kwa maandishi malalamiko yao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Pamoja na Necta kuwataka watumishi hao kwenda kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, walipofika katika ofisi hizo, malalamiko yao hayakupokelewa, kwa kile walichoelezwa kuwa NECTA inapaswa kuwapa taarifa ya nini cha kufanya na hawakuwa na taarifa hiyo bado mpaka jana.
Hata hivyo wakati hayo yakijiri, Waziri katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alilieleza gazeti hili mjini Dodoma jana kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, atalitolea ufafanuzi leo mjini humo.
Hivi karibuni Rais, John Magufuli alikabidhiwa taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma ambapo watumishi zaidi ya 9,932 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na alitangaza kuwafuta kazi na aliwapa siku 15, wawe wameondoka kazini, la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alichapisha sehemu ya kwanza majina ya watumishi hao katika vyombo vya habari na jana baadhi ya watumishi walianza kumiminika katika ofisi za Necta, kutaka kujua kasoro za vyeti vyao.
Katika kushughulikia tatizo hilo, Baraza hilo kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Dk Charles Msonde limewataka watumishi wa umma wenye malalamiko kuhusu matokeo ya uhakiki wa vyeti vyao, wawasilishe malalamiko yao kwa maandishi kwa Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia kwa waajiri wao na barua hizo za malalamiko, ziambatanishwe na nakala za vyeti husika.
Dk Msonde aliliambia HabariLeo kuwa wameamua kutumia njia hiyo, kwa kuwa Katibu Mkuu Utumishi ndie mwajiri na wao hufanya kazi na mwajiri na si mfanyakazi mmoja mmoja. Alisema ni ukweli ulio wazi kuwa watumishi wengi, walifanya ‘uchakachuaji’ katika vyeti vyao, walivyoviwasilisha awali wakati wa kuomba ajira na walipotakiwa kuleta vyeti halisi walibaini kuwa kuna tofauti.
“Kazi tuliyofanya sisi hapa baraza ni kuhakiki vyeti ambavyo tuliletewa na waajiri kuweza kubaini uhalali wake, lakini tuliyoyabaini ni mengi sana, watumishi wamekuwa wanafanya udanganyifu sana katika vyeti vyao,” alisema DkMsonde.
Aidha, kutokana na tangazo hilo, gazeti hili liliamua kufika katika Ofisi za Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kujionea baadhi ya watumishi wakifika kwa malalamiko, lakini lilipotaka ufafanuzi, lilielezwa kwamba msemaji ni Katibu Mkuu na yupo Dodoma.
Akizungumzia suala hilo, mmoja wa walalamikaji ambae hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema alifika NECTA saa 1 asubuhi na alikutana na walalamikaji wengi na mlinzi aliyekuwepo, aliwauliza nini tatizo na wakasema wanataka sehemu wanapohakiki vyeti.
“Mlinzi alituambia tusubiri saa 2:30 tutahudumiwa, lakini ilipofika saa 2:10 Ofisa mmoja wa NECTA alikuja na akabandika tangazo hilo kwenye ubao, baadae tukaona hamna msaada hapo mimi nikaamua kurudi ofisini nikaandika barua ya malalamiko nikapitisha kwa mwajiri wangu nikaelekea utumishi,” alisema.
Alisema alipofika Utumishi, aliwakuta walalamikaji wengine na baadae wakaenda chumba namba 6A, ambapo walimkuta ofisa mmoja (jina lake limehifadhiwa), akawaambia utaratibu haupo, hivyo kwa kuwa NECTA walipaswa wawasiliane nao kwanza.
“Sisi tulipofika alituambia kwamba Katibu Mkuu Utumishi hajatoa waraka na anatakiwa kwanza atoe maelekezo ili wajue wanayashughulikia vipi matatizo hayo na baadae alituonesha majina aliyokuwa nayo ni yale yaliyotoka kwenye gazeti na baraza ndiyo walipaswa kueleza kwamba yana tatizo gani,” alisema.
Kutokana na hayo, walalamikaji hao walionekana kukerwa na kauli hiyo na kudai kwamba wameonewa, kwa kuwa mtuhumiwa yeyote, lazima apewe muda wa kujitetea lakini wao hawakufanyiwa hivyo.
“Wote sisi tumeona majina gazetini na hatukuitwa kusikilizwa wakati ni haki yetu ya msingi, walipoona kama kuna makosa walipaswa watuite tujitetee lakini wao hawakufanya hivyo.
Sisi tulijitokeza tulitaka tuwe wa kwanza maana kuna wengi wanakuja hadi kutoka mikoani na tunaambiwa mwisho ni Mei 15…Tunaomba suala hili lishughulikiwe kwa haraka,” alisema.
Bungeni mjini Dodoma jana, Waziri anayeshughulikia utumishi wa umma, Kairuki alipoulizwa kuhusu malalmiko hayo, alisema leo Katibu Mkuu Utumishi atatolea ufafanuzi suala hilo.
Hata hivyo, baada ya Rais kupokea majina hayo ya waliobainika kuwa na vyeti feki, aliagiza kusitishwa mara moja mishahara yao, huku akiwataka waondoke kazini mara moja na watakaokaidi agizo hilo, watashitakiwa mahakamani.
Rais Magufuli alisema ni lazima watumishi hao, waondoke kwenye utumishi wa umma mara moja kutokana na kuisababishia serikali hasara kubwa. “Tena naagiza mshahara wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke kwenye utumishi wa umma, watakaokaidi watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na nafasi hizo 9,932 zitangazwe ili wasomi waweze kuziomba”.
Aidha, alitaka watumishi 1,538 ambao vyeti vyao vina utata mpaka Mei 15, mwaka huu, hatma yao ijulikane na kama wanajijua kuwa si wahusika wa vyeti hivyo waondoke mapema.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya wilaya ya Lindi mkoani Lindi imeanza kufanya mkakati wa kutafuta watumishi wa afya kwa ajili ya Zahanati za Mkanga II na Shuka kutokana na wahudumu wengi akiwemo dereva wa gari la wagonjwa, kuondolewa kazini mwishoni mwa wiki kutokana na kuwa na vyeti feki.
Hali ya huduma katika zahanati hizo inaelezwa kuwa si nzuri kutokana na kuondolewa kwa watoa huduma hao na tayari halmashauri imesema imenza kuchukua hatua. Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lindi, Samweli Warioba alithibitisha wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.
Alisema kuna tatizo la wahudumu wa afya kutokana na baadhi kuondolewa wa vyeti feki. Hata hivyo, hakufafanua kama wahudumu hao, atawapata wapi kwa haraka kutokana na zahanati hizo kutegemewa na wakazi wengi wa wilaya hiyo na maeneo ya karibu.
Ofisa wa Afya ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba wakati ambako watumishi hao hawajaondoka, bali kulikuwapo na upungufu wa watumishi wa afya zaidi ya 14, hata kabla ya Rais kutangaza walioghushi na kuondolewa.
Huko bungeni, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema taasisi hiyo haina mfanyakazi mwenye cheti feki hata mmoja, wafanyakazi wake kwa asilimia 100 wana vyeti halali vya taaluma zao na hiyo inatokana na utendaji bora wa mhimili huo.
Ndugai alisema hayo jana bungeni akizungumzia utendaji wa Bunge. Alisema Bunge ni miongoni mwa taasisi ambazo zina wasomi wengi, na kwamba ukiweka kwenye mizani itakuwa miongoni mwa tatu zenye wasomi wengi nchini.
Spika wa Bunge alitoa sifa hizo, kutokana na uvumi kuenea kwamba Bunge lina wabugne wengi wanaojua kusoma na kuandika tu, akasema ukiweka kwenye uwiano taasisi hiyo ina wasomi wengi mno.
Bunge lenye wafanyakazi 314, ni taasisi mojawapo ambayo ina wasomi wengi kama ukiweka kwenye mizani itakuwa miongoni mwa taasisi tatu za juu zenye wasomi wengi. Alisema hili ni bunge la wasomi, ukichukua maelezo yao hutaona kwamba kuna wabunge wanaojua kusomana kuandika tu, bali ni wasomi.
“Bunge lina wasomi wengi, hata kuzidi baadhi ya vyuo vikuu nchini, hakuna wafanyakazi ambao hawana elimu katika taasisi hiyo mchanganyiko ya wafanyakazi na wabunge,” alisema.
Spika Ndugai aliwapongeza wafanyakazi wa taasisi hiyo walioibuka kuwa wafanyakazi hasa mfanyakazi katika ofisi ya Katibu wa Bunge, Lydia Mpyiana ambaye ni mfanyakazi bora na atazawadiwa Sh milioni 10 kama motisha kwa utendaji wake. Imeandikwa na Mroki Mroki, Hellen Mlacky, Dar, Magnus Mahenge, Dodoma na Kennedy Kisula, Lindi.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini