Mbunge wa Mtama kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye ameeleza sababu ya yeye kuwa mkali wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambapo alikuwa miongoni mwa wabunge waliotaka bajeti ya wizara hiyo iongezwe ili kuweza kumtua mama ndoo kichwani.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Nape Nnauye amesema kuwa sababu ya yeye kuwa mkali na kupiga kelele kuhusu maji ni kutokana na maeneo ambayo wapigakura wake huchota maji.
Nape amechapisha picha zikionyesha watu wakichota maji katika visima na kuandika “Huku ndiko wanakochota maji baadhi ya wapiga kura wangu! Sasa mtanielewa kwanini napiga kelele na maji.”
Akichangia hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Nnauye alisema mabadiliko yanayofanywa na Rais Magufuli hayatakuwa na manufaa kama huduma za jamii hazitoboreshwa, huku akishauri bajeti hiyo kuongezwa.
Aidha, Nape Nnauye ameijia juu serikali kuhusu kupunguzwa kwa bajeti ya maji kutoka zaidi ya bilioni 900 kwa mwaka 2016/17 hadi kufikia bilioni 672.2 kwa mwaka 2017/18 ikiwa ni punguzo la asilimia 30.
Mbali na Nape, wabunge wengine waliopata nafasi ya kuchangia hotuba hiyo akiwemo, Zitto Kabwe, Mussa Mbarouk, Suleiman Bungara, Tunza Malapo na Dk. Mary Nagu waliunga mkono hoja ya bajeti ya wizara hiyo kuongezwa kwani maji ni tatizo linalowakumba wanachi wengi nchini.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini