Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Wadaiwa Sugu Tanesco Waorodheshwa, Wakatiwa Umeme


TAASISI za serikali mkoani Mbeya zinazodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), zimeanza kuonja uchungu wa kutajwa kwenye orodha ya wadaiwa sugu na baadhi kusitishiwa huduma.

Akizungumza na wandishi wa habari, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mbeya, Injinia Benedict Bahati, alizitaja taasisi hizo pamoja na madeni yao kuwa ni Jeshi la Polisi linalodaiwa zaidi ya Sh. milioni 700, Jeshi la Magereza (Sh. milioni 400) na Hospitali ya Kanda ya Rufani Mbeya (Sh. milioni 100).

Alizitaja taasisi zingine kuwa ni Jeshi la Kujenga Taifa (Sh. milioni 14) Jeshi la Wananchi (Sh. milioni 200) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) (Sh. milioni 70).
Injinia Bahati alisema baadhi ya taasisi hizo ambazo mwitikio wake wa ulipaji sio wa kuridhisha, likiwamo Jeshi la Polisi, zimesitishiwa huduma kwenye baadhi ya vitengo vyake ili kushinikiza kulipwa deni lao.

“Tayari kuna baadhi ya taasisi za serikali zenye madeni makubwa na mwitikio wake wa ulipaji sio mzuri, tumesitisha huduma mpaka watakapolipa, baadhi ya taasisi hizo ni Jeshi la Polisi na (TBC),” alisema Bahati.

Aidha, alisema mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira (Kiwira Coal mine), nao umeshasitishiwa huduma kutokana na kudaiwa zaidi ya Sh.bilioni 1.3.

Mhasibu wa Tanesco Mkoa wa Mbeya, John Makotwe, alisema tangu kuanza kwa operesheni ya kuwasaka wadaiwa sugu mkoani humo, wameshawasitishia huduma wateja 643.

Alisema baada ya operesheni hiyo mwitikio wa wadaiwa hao kulipa umekuwa mkubwa mpaka sasa wateja 153, wamelipa madeni yao na kurejeshewa huduma kwa masharti ya kufungiwa mita za Luku na kuondoa zile za zamani.

Alisema kitendo cha wateja hao kutolipa madeni yao kwa muda mrefu, kinasababisha shirika hilo kushindwa kuwaunganishia wateja wapya na uendeshaji wa shughuli zingine za shirika.

“Uendeshaji wa Shirika unategemea mauzo ya huduma yetu ambayo ni umeme, hivyo kitendo cha taasisi hizo kushindwa kulipa madeni kwa muda mrefu kinakwamisha shughuli za shirika,” alisema Makotwe.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa taasisi hizo walikiri kudaiwa na shirika hilo huku wakieleza taratibu zinazofanyika ndani ya taasisi zao kulipa madeni hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alikiri kudaiwa deni na Tanesco pamoja na kusitishiwa huduma hiyo kwenye baadhi ya vitengo na kwamba wao kama taasisi wanadaiwa kama ilivyo kwa taasisi zingine.

Alisema kwa sasa tayari wanaendelea na taratibu za kulipa deni hilo ili waendelee kuipata bila usumbufu.
Naye Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kijida Paulo, alikiri kuwapo kwa deni la Sh. milioni 400 na kwamba hawajasitishiwa huduma kutokana na kuwa na mawasiliano ya karibu na Tanesco kuhusu hatua za kulipa deni.
Alisema mpaka sasa taratibu zinafanyika na uongozi wa juu kulipa deni hilo kupitia Hazina na kwamba huduma zingine walizokuwa wanadaiwa ikiwemo maji wameshaletewa fedha kwa ajili ya kulipa.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017