Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Wakristo 23 Wauawa Wakienda Kanisani Kwa Maombi


Watu takriban 23 wameuawa na wengine 25 kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kufyatulia risasi waumini wa kanisa la Coptic waliokuwa wakisafiri kwa kutumia basi katikati mwa Misri, vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo vimesema.

Kisa hicho kilitokea katika mkoa wa Minya, takriban kilomita 250 (maili 155) kusini mwa Cairo, basi hilo lilipokuwa linawasafirisha kwenda kanisani.

Kumetokea visa kadha vya waumini wa kanisa la Coptic kushambuliwa, mashambulio ambayo kundi la Islamic State limedai kuhusika.

Mashambulio mawili ya mabomu ya kujitoa mhanga katika makanisa Tanta na Alexandria mnamo 9 Aprili yalisababisha vifo vya watu 46.



Waumini hao waliuawa walipokuwa wakisafiri kwenda kanisa la Mtakatifu Samuel kuomba.
Basi lao lilikuwa katika msafara mdogo wa magari na taarifa zinasema gari hilo lilisimamishwa na watu kati ya wanane na kumi waliokuwa wamevalia sare za kijeshi.

Watu hao wenye silaha walifyatulia risasi basi hilo kwa kutumia bunduki za rashasha kisha wakatoroka kwa kutumia magari matatu ya 4x4.

Afisa Mkristo kutoka Minya Ibram Samir ameambia gazeti la New York Times kwamba kulikuwa na watoto kwenye basi hilo na ni miongoni mwa waliofariki.

Gavana wa Minya Essam al-Bedawi amesema maafisa wa usalama walifika eneo hilo na wanaweka vizuizi kwenye barabara hiyo ya kulekea kanisa la Mtakatifu Samuel pamoja na kufanya msako mkali.

Wakristo wa Coptic hujumuisha asilimia 10 ya raia wote 92 milioni wa Misri.
Mashambulio ya mwezi jana yalimfanya Rais Abdul Fattah al-Sisi kutangaza hali ya hatari ya miezi mitatu kote nchini humo na kuahidi kuchukua hatua kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu, wengi ambao hutoka maeneo ya kaskazini ya Sinai.

Lakini wengi wa waumini wa Coptic wamekuwa wakilalamika kwamba serikali haifanyi juhudi za kutosha kuwalinda, anasema mwandishi wa BBC aliyepo Cairo Orla Guerin.

Kwa sasa kuna hali ya wasiwasi miongoni mwa Wakristo ambao wanahisi kwamba wanawindwa, anasema.

Kanisa la Coptic ni gani?
Kanisa la Coptic ni la Kiothodoksi na ndilo kanisa kuu la Kikristo nchini Misri.
Ingawa wengi wa waumini wa Coptic huwa Misri, kanisa hilo lina waumini karibu milioni moja nje ya nchi hiyo.

Wengi wa waumini wa kanisa hilo huamini kwamba asili ya kanisa lao ni mwaka 50 AD (Baada ya kuzaliwa kwa Kristo) pale Mtume Mark alipozuru Misri.

Mkuu wa kanisa hilo huitwa Papa na huchukuliwa kuwa mrithi wa Mtakatifu Mark.
Kanisa hilo lilijitenga na Madhehebu mengine ya Kikristo katika Mkutano wa Chalcedon (451 AD) baada ya mzozo kuhusu sifa za utu na umungu za Yesu Kristo.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017