Na Salum Vuai, MAELEZO
WASANII Hammer Q na Mossi Suleiman, wameingia matatani baada ya kutajwa kwa wizi wa wimbo wa kikundi cha taarab Culture Musical Club cha Zanzibar.
Hali hiyo imejitokeza kufuatia wasanii hao kuimba na kurekodi wimbo uitwao ‘Ukewenza’ ulioimbwa kwa pamoja na wasanii wakongwe Bi. Mwapombe Hiyari Mtoro na marehemu Bwana Sami Haji Dau tangu Culture ikiitwa Mila na Utamaduni.
Katibu wa Culture Musical Club Taimour Rukun Taha amesema uongozi wa klabu hiyo unakusudia kuwachukulia hatua za kisheria wasanii hao kwa kitendo chao cha kuimba na kurekodi wimbo huo ambao ni mali ya klabu yake bila ya idhini.
Akizungumza makao makuu ya klabu hiyo Vuga mjini Zanzibar, Rukun alisema, kitendo kilichofanywa na wasanii hao kinakwenda kinyume na sheria ya hakimiliki Zanzibar, Tanzania na ile ya kimataifa.
Aidha alisema, kwa mujibu wa katiba ya klabu yao, ni marufuku kwa mtu au kikundi chochote kutumia kibiashara wimbo uliotungwa, kutiwa muziki na kuimbwa klabuni humo bila ya makubaliano kati ya pande hizo.
“Tumesikia na kushuhudia rekodi ya wimbo wetu wa ‘Ukewenza’ ambao asili yake uliimbwa kwa pamoja na Bi. Mwapombe na marehemu Sami Haji Dau miaka mingi nyuma, ukiimbwa na Hammer Q na Mossi Suleiman. Ni wapi walikopata idhini kwani sisi wamiliki hawakuja kutuomba wala hakuna kati yetu aliyewaruhusu,” alifafanua Rukun.
Kimsingi, Katibu huyo alisema uongozi na wanachama wa klabu hiyo wanasikitishwa na kulaani kitendo chochote cha kurekodi na kuuza nyimbo za wasanii au vikundi vyengine mbali na Culture, kufanywa na watu wengine bila ya makubaliano.
Alieleza kuwa mbali na kurekodiwa, pia wanakerwa na mtindo wa kuzibadilisha nyimbo hizo na kuongezewa vionjo ambavyo awali havikuwemo, ikiwemo vibwagizo vilivyopewa jina la ngoma chini jambo alilosema klabu yake haifanyi.
Alisema wapo baadhi ya wasanii ambao wanaendeleza mtindo wa kuzipiga nyimbo za Culture katika shughuli mbalimbali na pia kuthubutu kuzirekodi na kuuza wakinufaika binafsi.
“Hii ni dhuluma kwani nyimbo hizo ni mali yetu na sisi ndio wenye hakimiliki na kama mtu anataka kuzitumia lazima afuate taratibu za kisheria,” alisisitiza.
Kwa hivyo, amewatumia salamu watu wote na vikundi vinavyojinufaisha kwa nyimbo za klabu hiyo, kujiandaa kukabiliana na mkono wa sheria, akisema wakati wa kuwafumbia macho umekwisha, kwani hata wanachama wanaumizwa na vitendo hivyo ambao kimsingi ndio wenye mali.
Katika siku za hivi karibuni, Hammer Q na Mossi Suleiman wamekuwa wakisikika na kuonekana kwenye mitandao ya kijamii wakiimba wimbo wa ‘Ukewenza’ ambao wengine huuita ‘Mke wa awali, wakitumia vyombo vya kisasa badala ya vile vya asili kama ulivyorekodiwa katika uasili wake.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini