BAADA ya muda mrefu Yanga kuwa mbali na mwenyekiti wao, Yusuf Manji kutokana na kukumbwa na matatizo yake binafsi, taarifa zilizoibuka zinadai kuwa tayari amerejesha majeshi yake kwa kuiunga mkono klabu hiyo kwa kufanya nao mawasiliano ya karibu kila siku kama ilivyokuwa awali.
Mwenyekiti huyo, amefikia hatua hiyo katika kuhakikisha wanaubakiza ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Yanga, hivi sasa tayari imefanikiwa kuwaondoa watani wao Simba kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu kwa kuwa na pointi 62, sawa na Simba wakitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo tumezipata kutoka ndani Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, kwenye kila mechi ya ligi kuu ambayo Yanga wanaicheza, mwenyekiti huyo anawatengea kitita cha Sh milioni 20, kama fedha ya morali kuhakikisha wanapambana ndani ya uwanja ili waubakize ubingwa huo.
Mtoa taarifa huyo alisema, fedha hizo zimeanza kumwagwa kuanzia mechi iliyopita ya ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons waliyoshinda mabao 2-0 na nyingine dhidi ya Kagera Sugar waliyoshinda 2-1, zote zilichezwa Uwanja wa Taifa, Dar.
“Naamini kabisa wengi hawajui kwa nini wachezaji wa Yanga sasa wameamka kuliko mwanzo, kikubwa ninachoweza kukudokeza ni kwamba, tayari Manji amekuwa akiwasiliana na baadhi ya wachezaji wake wakongwe kwa kuwapigia simu na kuwataka wapambane huku wakijua yeye yupo nyuma yao kwani matatizo yake yamemalizika.
“Kikubwa anataka kuona wachezaji wakipata huduma zote walizokuwa wakizipata awali bila kupungua kitu.
“Watu wengi hawajui kinachoendelea kati ya mwenyekiti na timu, ila kikubwa mimi nikuhakikishie kuwa Manji amerejea kwa asilimia zote, hivyo habari ya bakuli lililokuwa likitembea, siyo ishara ya kwamba hayuko na timu, sema hiyo ni sehemu ya kutafuta fedha nje ya mfuko wa klabu na huduma zake za mwanzo, kuna mambo makubwa mengi aliyowaahidi ikiwa ni pamoja na kutowaacha wachezaji wote ambao mikataba yao inamalizika,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema:
“Manji yupo juu yangu na yeye ni mwenyekiti wangu, nisingependa nizungumzie suala la mtu, kwa hiyo ni vyema angetafutwa Manji mwenyewe aweze kulizungumzia suala hilo.”
Tulifanya jitihada za kumtafuta Manji siku nzima ya jana lakini simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikan.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini