Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Elisha Mghwira amepinga uamuzi wa chama hicho kumvua wadhifa huo mara tu baada ya kuapishwa kuuongoza mkoa wa Kilimanjaro.
Baraza la Uongozi la ACT-Wazalendo lililokutana Juni 7 mwaka huu ikiwa ni siku moja tangu Anna Mghwira alipoapishwa Ikulu Juni 6, liliadhimia kumvua uongozi wa chama kwa madai kuwa asingeweza kutekeleza kwa uafnisi majukumu yake mapya na yale ya chama.
Anna Mghwira ambaye alikuwa mgombea pekee mwanamke katika uchaguzi mkuu wa 2015 aliyasema hayo jana alipofika ofisini kwake kwa mara ya kwanza na kupokewa watumishi wa ofisi yake ambapo alisema, Baraza la Uongozi halina mamlaka ya kumuondoa kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama.
Alisema kuwa waliomvua madaraka ni Baraza Kuu la Chama lakini mamlaka ya kumpumzisha mwenyekiti yamekasimiwa kwa Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa katiba ya ACT Wazalendo.
“Niliwasiliana na muasisi wa chama, Zitto Kabwe nikamwambia nipo kwenye pilika pilika za kuapishwa hivyo asubiri hadi Juni 15 ambapo ningekutana nao katika Mkutano Mkuu wa chama, lakini baraza limeamua kufanya maamuzi ya haraka,” alisema Anna Mghwira.
Akizungumzia uamuzi huo alisema hata Rais Magufuli ni Mwenyekiti wa CCM, lakini bado anatumikia nafasi yake ya urais. Anna Mghwira amekuwa kiongozi wa kwanza wa chama cha upinzani ngazi ya juu kuteuliwa serikalini.
Anna Mghwira aliyeteuliwa kushika nafasi iliyoachwa wazi na Meck Sadick alisema uamuzi huo kwa upande mwingine umempunguzia majukumu.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini