Mkemi alikumbana na kadhia hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar, muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Sportpesa Super Cup ambapo Yanga ilikubali kichapo cha penalti 4-2 kutoka kwa AFC Leopards baada ya matokeo ya 0-0 katika dakika 90.
Mashabiki hao walidai kwamba Mkemi amekuwa akiongea maneno mabaya jambo ambalo limesababisha hadi mwenyekiti wao huyo kukaa pembeni na kuiacha timu hiyo, huku yeye akishindwa kuiratibu vyema timu hiyo ikiwa na kutofahamu hatma za nyota wao ambao wanamaliza mikataba.
Kutokana na mashabiki hao kutaka kumvaa mjumbe huyo wa Yanga, polisi waliokuwa uwanjani hapo walilazimika kumuepusha na kipigo na kumuondoa Mkemi kutoka jukwaani hadi lilipokuwa gari lake.
Championi Ijumaa, limezungumza na Mkemi ambapo anasema: “Mimi nawashangaa mashabiki hawa wanaotaka kunipiga kwani Manji kuachia ngazi imetokana na sababu zake mwenyewe na siyo mimi niliyesababisha yeye kujitoa ndani ya timu.”
YANGA YATOLEWA SPORTPESA SUPER CUP
Yanga ambayo ilikuwa timu pekee kutoka Tanzania iliyosalia kwenye michuano hiyo, iliungana na Simba, Singida United na Jang’ombe Boys kuyaaga mashindano hayo yaliyoanza kwa kuzishirikisha timu nane.
Katika mikwaju ya penalti, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Obrey Chirwa, ndiyo waliopata kwa upande wa Yanga, huku Said Juma Makapu na Said Mussa, wakikosa. Ian Otieno, Bernard Mango, Kateregga Allan na Whyvonne Isuza waliifungia AFC Leopards, huku Ingotsi Marselas akikosa.
Katika mchezo wa mwisho wa nusu fainali, Gor Mahia iliifunga Nakuru All Stars mabao 2-0 yaliyofungwa na Meide Kagere na George Odhiambo. Kwa matokeo hayo, AFC Leopards itavaana na Gor Mahia kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa Jumapili hii.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini