VIGOGO wa Wizara ya Nishati na Madini, wanaokabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusaidia familia zao zipate mishahara kwa sababu wanahitaji huduma.
Washitakiwa hao ni Mkurugenzi wa Tathmini, Archard Kalugendo (49) na Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu (50). Akiwasilisha maombi yao hayo jana, Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko alimwomba Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage mahakama isaidie familia zao kupata mishahara kwani wana watoto wanaohitaji huduma, wanaumwa.
“Tungeomba washitakiwa wapate dhamana lakini Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ameweka zuio. Tunaomba wapewe mishahara yao hata kwa kupitia dirishani halafu waendelee kushikilia akaunti zao,” aliomba Nkoko.
Alitoa ombi hilo baada ya Wakili wa Serikali, Saimon Wankyo kudai kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika. Wankyo alimshauri Wakili Nkoko kuandika barua kwa DPP ili ashughulikie suala hilo.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini