MUDA mchache baada ya kushuhudia timu yake ikipata bao la pekee katika dakika za nyongeza dhidi ya Tanzania Prisons juzi, Kocha wa Singida United, Hans van der Pluijm, alijikuta akiingizwa mjini na vibaka kwa kuibiwa mkoba wa fedha wakati akishangilia bao hilo.
Pluijim aliibiwa mkoba huo uliokuwa na simu aina ya Sumsung Pro 9 yenye thamani ya Sh. 1,575,700, pochi ('wallet'), leseni ya udereva kwa nchi mbili Tanzania na Ghana, fedha za Dola 100 za Marekani, fedha taslimu Sh. 200,000 za Tanzania na funguo za gari lake aina ya Prado.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi, alisema baada ya ushindi huo, mashabiki walishangilia sana kiasi cha mhalifu kutumia mwanya huo kuiba mkoba wa kocha huyo hivyo kulazimika kuripoti polisi na msako mkali kuanza.
Askari wakiongozwa na taarifa za kitengo cha makosa ya mtandao kwa kutumia namba ya simu ya Pluijim iliyokuwamo kwenye mkoba, walifanikiwa kupata begi hilo likiwa limetupwa eneo la mtaa wa Kindai baada ya mwizi kubaini anafuatiliwa na polisi.
Mbughi alisema kweye mkoba huo polisi walifanikiwa kukuta vitu vyote isipokuwa fedha ambazo mwizi alitoweka nazo.
Pluijim alipatiwa vitu vyake vyote isipokuwa fedha, lakini amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako kumbaini aliyehusika na uhalifu huo.
Aidha, jeshi hilo limetahadharisha wapenzi na mashabiki wa soka kujihadhari dhidi ya wezi wanaoingia uwanjani kwa nia mbaya huku wakikusudia kufanya uhalifu wakati wa kushangilia ushindi au bao linapofungwa.
Katika mchezo huo Singida United ilipata bao pekee dakika sita za nyongeza kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Elinywesia Sumbi, ‘Msingida’ aliyeingia uwanjani dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Deus Kaseke.
Chanzo Nipashe
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini