SIKU chache baada ya familia ya mwanamuziki, Mbaraka Mwinshehe, kutoa ruhusa kwa Vanessa Mdee kunakili vionjo vya wimbo wa baba yao (Jogoo la Shamba) na kuviweka kwenye wimbo wake wa Pumzi ya Mwisho, msanii wa Singeli, Aman Hamis, amejikuta matatani baada ya kunakili vionjo vya wimbo wa nguli huyo wa dansi bila kuitaarifu familia.
Mtoto wa Mbaraka Mwinshehe, Kipande Mbaraka, ameliambia Papaso la Burudani kwamba, wao na bendi ya Morogoro Jaz wana hakimiliki ya wimbo huo na endapo watashindwa kuelewana, basi watamburuza mahakamani msanii Man Fongo.
“Sisi tunahitaji kuzungumza naye, tusipofikia mwafaka basi sheria itachukua mkondo wake, wimbo ameutumia umekaa vizuri ila tatizo hatukufanya makubaliano naye,” alisema Kipande.
Man Fongo naye ameliambia Papaso la Burudani: “Nawaomba sana ndugu zangu, mimi sikuyajua hayo wala wasidhani sisi wanamuziki wa Singeli tuna pesa kama Bongo Fleva, ndiyo kwanza tunapambana kuufikisha muziki mbele na niliimba ili na wazee nao wasikilize Singeli wasidhani ni muziki wa wahuni na vibaka kama inavyodhaniwa,” alisema Man Fongo aliyepata matatizo hayo baada ya kutoa wimbo unaoitwa Lau Nafsi.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini