Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Simba Sc Waanza Kuhisi ‘Dalili Mbaya’ Suala La Mohammed Fakhi


KATIKA kile kinachoashiria kuanza kuhisi dalili mbaya upande wao juu ya kinachoendelea kwenye kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), klabu ya Simba imeanza kutaharuki.
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana ilishindwa kuamua juu ya sakata la beki Mohammed Fakhi kuichezea Kagera Sugar dhidi ya timu yake ya zamani, Simba akiwa ana kadi tatu za njano na kulisogeza mbele suala hilo hadi leo.
Kikao hicho kilichoanza Saa 4:00 asubuhi katika hoteli ya Protea, Masaki, Dar es Salaam kilifungwa Saa 2:05 usiku na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa akasema kitaendelea leo kwa sababu wanahitaji vielelezo na ushahidi zaidi ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.
Dalili siyo nzuri; Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange 'Kaburu' na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe (kulia). Leo watasema nini? 

Lakini wakati taratibu hizo zikiendelea, Simba wanatarajiwa kuwa na mkutano na Waandishi wa Habari Saa 5:30 asubuhi ya leo kuzungumzia suala hilo hilo.
Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara jana usiku ilisema; “Klabu ya Simba inapenda kuwaarifu waandishi wa habari, itakuwa na mkutano wake 'Maalum' na wana Habari kesho saa tano na nusu asubuhi ya tarehe 19-4-2017. Mkutano huo unalenga kutoa ufafanuzi mpana wa kinachoendelea kwenye mchezo wa soka unaopendwa na kushabikiwa sana kote nchini na duniani kwa ujumla,”. 
Taarifa hiyo ilitoka muda mfupi tu baada ya kikao Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kuahirishwa jana.
Kikao hicho kinafuatia Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki aliiomba TFF kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa siku wanaifunga Simba 2-1.
Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Utata upo katika mchezo wa Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kati ya wenyeji Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam, ambao inadaiwa Fakhi alionyeshwa kadi ya njano wakati klabu yake inapinga.
Viongozi wa klabu za Simba, African Lyon, Kagera Sugar, marefa na Fakhi mwenyewe walihojiwa jana Protea kwa nyakati tofauti na taarifa zinakinzana.
Baadhi ya waliohojiwa wanasema kweli Fakhi alikuwa ana kadi tatu, lakini wengine wamesema mchezaji huyo hakuwa na kadi tatu.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017