Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

MUHIMU:Hivi Ndiyo Earphone Zilivyo Hatari Kwenye Masikio


Kundi kubwa la watu watumiaji wa spika ndogo za masikioni (earphone), hasa wanahabari na wanafunzi, wako hatarini kupata magonjwa mbalimbali yanayotokana na vijidudu vinavyoambukiza, uchunguzi umebaini.
Uchunguzi huo umebaini kuwa ni jambo lililozoeleka kwa wanahabari wanapokuwa vyumba vya habari au maofisini, kuazimana spika hizo bila kuchukua tahadhari za kiafya.
Mbali na kundi hilo, kundi kubwa la vijana wadogo, hasa wanafunzi, pia liko katika hatari ya kupata maambukizo ya magonjwa ya masikio kutokana na mazoea hayo ya kuchangia matumizi ya spika hizo.

Watu mbalimbali waliohojiwa, wameelezea kutoelewa athari zinazoweza kusabishwa na kuchangia earphone ambazo huweza kubeba magonjwa ya ngozi na yale ya masikio kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Dk Kareem Segumba alisema uchangiaji wa ‘earphone’ si jambo zuri kwa kuwa husababisha maambukizi ya magonjwa mbalimbali kutoka kwa mtu mmoja aliyeathirika kwenda kwa mwingine.
“Kitaalamu tunasema anapata contagious (maambukizi) ya magonjwa ya sikio toka kwa mgonjwa. Magonjwa haya ni pamoja na fungus ya masikio,” alisema Dk Kareem.
Dk Kareem, ambaye amehudumu katika hospitali mbalimbali nchini, alitaja magonjwa mengine kuwa ni maambukizi ya sikio sehemu ya mzunguko na maambukizi kwenye ngoma ya sikio.

“Mara nyingi mtu anayeumwa fangasi ya sikio au kutokwa na majimaji kidogo kabla ya kugeuka usaha huwa hawajitambui. Wengi wanajua baada ya kuona usaha,” alisema.
“Si desturi nzuri kuchangia earphone na mtu yeyote kwa kuwa madhara yake ni makubwa na hasa ukizingatia masikio yako karibu sana na ubongo na huenda ukapata maambukizi kupitia mishipa.
“Mishipa ya damu inapeleka vijidudu vya ugonjwa kwenye ubongo na hatimaye kutokea athari nyingine kama uziwi, kupoteza nguvu ya kuona na matatizo kwenye uti wa mgongo.”
Mpigapicha wa kituo cha televisheni cha ITV mkoani Kilimanjaro, Robert Minja alikiri watu wengi hususan wanahabari wamekuwa na tabia ya kuchangia earphone, kwa vile hawajui madhara.

“Hilo la ku- share earphone (kuchangia) lipo sana na inavyoonekana watu wengi hawajui madhara yake. Tunaona ni mambo ya kawaida lakini kiukweli hii tabia ina madhara ya kiafya,” alisema.
Maulid Rashid, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (Smmuco) alisema tatizo la kuchangia vifaa hivyo ni kubwa chuoni hapo.
“Ni kweli wanafunzi wengi wanachangia hizo earphone. Nafikiri wanaofanya hivyo hawana uelewa kuwa kuna madhara. Yaani hili ni tatizo kubwa si kwa wanafunzi tu hata watu wa kawaida,” alisema.


Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017