Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola amesema kuwa majeshi ya usalama hapa nchini yamesahaulika na yanachukuliwa kama ni ya kawaida huku watendaji wake wakichukuliwa kama hawana taaluma hiyo (professionalism).
Lugola ameyasema hayo Bungeni wakati akichangia hotuba ya Waziri ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Lameck Nchemba kuhusu bajeti ya wizara hiyo.
“Majeshi ya Polisi, Magereza, Uhamiaji na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji yamedharaulika, yanachukuliwa kama ya kawaida na ya ‘miujiza’.
“Kama hatutawekeza kwenye majeshi yetu hatuwezi kupunguza uhalifu wala kuleta nidhamu kwenye nchi yetu.
“Askari wetu tunawapa posho ndogo, kuigawa kwenye matumizi yake ya kila siku inakuwa vigumu ikilinganishwa na kazi wanazofanya.
“Hawa wanaovamiwa kwenye mabenki na kwenye doria, unakuta askari ana stress, ana njaa, anapiga miayo tu, matokeo yake anayang’anywa silaha. Tunahitaji kuboresha mafunzo yao,” alisema Lugola.
Akizungumzia askari wanaojificha vichakani Lugola amesema:
“Zaidi ya miaka kumi sasa hakuna mafunzo ya trafiki tena hapa nchini, unakuta trafiki wanachoropoka ghafla kutoka vichakani wanakusimamisha, hao hawana mafunzo ya kutosha,” alisema Lugola.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini