Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Malaria Yamlaza Tshishimbi Akosa Mazoezi, Tambwe Arejea


WAKATI mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe amefanya mazoezi mepesi leo, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi hakutokea kabisa.

Yanga SC imefanya mazoezi leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Jumapili.

Tambwe ambaye hajacheza kabisa msimu huu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, alikuwepo leo na kufanya maozezi ya kukimbia pole pole na kunyoosha viungo.

Majeruhi mwenzake, kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko hakuwepo kabisa, sawa na wachezaji wote waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars nchini Benin.

Tshishimbi naye hakuwepo leo na Daktari wa timu, Edward Bavu akasema kwamba mchezaji huyo wa zamani wa Mbabane Swallows ya Swaziland anasumbuliwa na homa ya Malaria.

Bavu alisema Tshishimbi anaweza kurudi mazoezini kesho sambamba na wachezaji waliokuwa na Taifa Stars nchini Benin.  

Taifa Stars imerejea nchini alfajiri ya leo kutoka Benin ambako Jumapili ilitoa sare ya 1-1 na wenyeji katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ambao ulionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walitangulia kwa bao la la penalti ya utata ya Nahodha wao, Stephane Sessegnon kipindi cha kwanza, kabla ya Elias Maguli kuisawazishia Stars kipindi cha pili.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017