Papy Tshishimbi.
WAKATI wapenzi na mashabiki wa soka mkoani Singida wakijiandaa kuiona kwa mara ya kwanza timu yao ya Singida United ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Namfua dhidi ya Yanga kesho Jumamosi, mashuti ya Papy Tshishimbi yamezua balaa ndani ya timu hiyo.
Jumamosi iliyopita, Tshishimbi alipiga mashuti mawili ya nguvu alipokuwa akiitumikia Yanga dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Hata hivyo mashuti hayo yalipanguliwa kwa ufanisi mkubwa na kipa wa Simba, Aishi Manula ambaye alifanya kazi kubwa katika mechi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa Singida United wanaumiza vichwa vyao kila wanapomfikiria kiungo huyo wa Yanga, ambaye hivi sasa ndiye gumzo kubwa hapa nchini kutokana na uwezo wake mkubwa alioonyesha dhidi ya Simba, Jumamosi iliyopita.Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, ameliambia Championi Ijumaa kuwa Tshishimbi ndiye mchezaji ambaye wanamhofia zaidi katika mechi hiyo japokuwa wanaamini kuwa kocha wao mkuu raia wa Uholanzi, Hans van Der Pluijm atakuwa ameshamuandaa mtu maalumu wa kukabiliana naye uwanjani.
“Sisi kama uongozi tumejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo lakini pia mambo yote ya kiufundi ndani ya uwanja, pia kocha wetu, Pluijm amejipanga vizuri.
“Hata hivyo, mchezaji ambaye tunamhofia zaidi kwa upande wa Yanga ni Tshishimbi kwani ni mchezaji mzuri tangu amejiunga na timu hiyo ndiye injini yao, tukifanikiwa kumdhibiti huyo basi kazi itakuwa nyepesi kwa upande wetu,” alisema Sanga.
Hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa timu hizo mbili kukutana mwaka huu, ambapo mara ya kwanza ilikuwa katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Wakati huohuo, Pluijm amezungumza na Championi Ijumaa juu ya mchezo huo ambapo amesema: “Upande wetu sisi tuko vizuri kabisa na tupo tayari kwa ajili ya pambano hilo, na nina uhakika mkubwa kwamba tutaonyesha upinzani mkubwa kwa wapinzani wetu, kutokana na sisi kuwa nyumbani lakini tunawajua vyema wapinzani wetu.
“Tunaingia kwenye mechi hii tukiwa tunawajua vizuri wapinzani wetu kwa sababu wengi kabla ya kuja huku tulikuwa pale, kwa hiyo hapo kuna urahisi mkubwa wa sisi kupata matokeo mbele yao.”
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini