WATU 25 wa familia moja wamejeruhiwa katika ajali baada ya lori kugongana na basi walilokuwa wakisaifiria.
Ajali hiyo ilitokea jana wilayani Mvomero ambako basi hilo lililogongana na lori namba T 712 CHQ Scania likiwa na tela namba T 591 BYS ambalo lilikuwa likijaribu kuyapita magari mengine.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema baada ya lori hilo kushindwa kuyapita magari hayo, liligonga basi la Karim Trans namba za usajili T 465 DGQ.
Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva Mathew Benedict, likitokea Turiani wilayani Mvomero kwenda mjini Morogoro.
Lilikuwa limekodiwa na familia ya Matesa ambayo ilikuwa ikienda kumaliza msiba wa baba yao.
Kamanda Ulrich alisema majeruhi wengine walitibiwa na kuruhusiwa huku 25 wakilazwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro kwa matibabu zaidi .
“Tumepokea majeruhi wengi lakini wengi wao hawajaumia sana na wametibiwa na kuruhusiwa,” alisema Kamanda Matei
Aliwataja baadhi ya majeruhi walioumia katika ajali hiyo kuwa ni Odilia Ipoliti, Zainabu Mahamba, Shukuru Mrisho, Sauda na Anna ambao wametambulika kwa jina moja.
Kamanda Matei alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa akijaribu kuyapita magari mengi kwa pamoja na kusababisha ajali hiyo.
“Tunashukuru Mungu hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hii.
“Na tunawaomba madereva wote kuwa makini hasa wanapokuwa barabarani wanapoendesha vyombo vya moto,” alisema Kamanda Matei.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini