Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Siri Ya Rais Magufuli Kutengua Uteuzi Wa IGP Ernest Mangu



Ikiwa bado wananchi wanaendelea kuumiza kichwa kufahamu aliyeko nyuma ya matukio ya mauaji yanayoendelea mkoani Pwani, Rais Magufuli na Amiri Jeshi Mkuu ametengua uteuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, jeshi ambalo ndilo lenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

Uamuzi huu wa Rais Magufuli umekuja ikiwa tayari watu zaidi ya 30 wameuawa katika Wilaya za Kilwa, Rufiji, Kibiti na Mkuranga ambapo miongoni mwa waliouawa wamo pia Askari Polisi wanane.

Rais Magufuli ametengeua uteuzi wa IGP Ernest Mangu na kumteua Simon Sirro kushika nafasi hiyo.
Licha ya kuwa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu haikueleza sababu ya mabadiliko hayo, lakini inaaminika kuwa utenguzi huo umetokana na mfululizo wa matukio ya mauaji katika wilaya hizo yaliyohusisha wananchi, viongozi wa serikali na Askari Polisi wa Tanzania na hadi sasa wahusika hawajakamatwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro kuwa IGP akichukua nafasi ya Ernest Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Aidha, wengine wamedai kuwa uamuzi huo pia huenda umechangiwa na kauli ya Mangu aliyoitoa siku za karibuni kuwa, vitendo vya Polisi kuwakamata waandishi wa habari wakiwa kazini, si msimamo wa Jeshi hilo.
Ernest Mangu aliteuliwa kuwa IGP na Rais mstaafu, Dkt Jakaya Kikwete mwaka 2013 akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Saidi Mwema ambaye alistaafu.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017