Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekwama kusikiliza kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya bangi inayomkabili msanii wa filamu Wema Sepetu na wenzake kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde, jana alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kuwa shauri hilo lilipaswa kuanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba lakini hayupo.
Mkunde alidai kuwa hakimu Simba ameanza likizo, hivyo anaomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa alisema kuwa shauri hilo limeahirishwa hadi Julai 10 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Mbali ya Wema katikakesi hiyo, washitakiwa wengine ni Angelina Msigwa na Matrida ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa hizo. Kwa pamoja inadaiwa kuwa walitenda kosa hilo Februari 4 mwaka huu katika makazi yao Kunduchi, Ununio ambapo walikutwa na misokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08
Shtaka la pili linamkabili Wema Peke yake ambapo inadaiwa kuwa tarehe tofauti kati ya Februari 1 na 3 mwaka huu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es salaam alitumia dawa za kulevya aina ya bangi. Akiwasomea maelezo ya awali, Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai kuwa Wema alikuwa ni miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Alidai kuwa Februari 3 mwaka huu alijipeleka Kituo Kikuu cha Polisi Kati ambako alikamatwa na Februari 4 mwaka huu ukaguzi uliofanyika nyumbani kwake ambapo kulipatikana vitu vinavyodhaniwa kuwa dawa za kulevya.
Kakula alidai kuwa ukaguzi huo uliofanyika mbele ya msanii mwenyewe , polisi na mashahidi huru na Februari 6 mwaka huu, vitu hivyo vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, na Februari 8 Mkemia alitoa taarifa ya uthibitisho juu ya vielelezo hivyo kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 1.08
Alidai kuwa Februari 8 mwaka huu Wema alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa mkojo ambapo uchunguzi ulieleza kuwa mkojo wa msanii huyo ulikuwa na bangi.
Katika maelezo hayo ya awali, Wema alikubali majina yake, mahali anapoishi na kwamba alikuwa miongoni mwa waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kujihusisha na dawa za kulevya. Pia, alikubali kujipeleka polisi huku akikana maelezo mengine.
Washitakiwa wengine walikubali majina yao na kuwa wafanyakazi wa wema.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini