Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Madudu Ya Kitisha Yaibuliwa Uhamiaji


KAMISHNA JENERALI WA IDARA YA UHAMIAJI DKT. ANNA MAKAKALA.

TAARIFA za fedha za Idara ya Uhamiaji nchini zimebainika kuwa na madudu hasa katika utoaji wa visa uliogubikwa na mazingira ya rushwa na upotevu wa mapato.

Madudu hayo yalibainishwa jana na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), wakati ikihoji Idara hiyo, kuhusu hoja za ukaguzi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/16.

Katika mahojiano hayo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Tambwe, alisema ni aibu idara hiyo kugubikwa na mazingira ya rushwa.

“Kwa mfano wa wawekezaji kutoka China walifika kwa ajili ya kuweka makubaliano ya kuwekeza kiwanda cha kusindika Tumbaku mkoani Tabora, lakini walirudia katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam baada ya kukosa visa kwa kuwekewa mazingira ya rushwa,” alisema.

Kadhalika, alisema pia kuna wageni wa wadau wa Simba ambao walifika nchini wakitokea Ivory Coast, lakini wakataka visa, ili kwenda Vietnam, lakini idara hiyo iliwanyima na kuwataka kurudi nchini kwao kwenda kupata visa za kuingia nchini Vietnam.

Tambwe alisema kuna mazingira ya rushwa na kwamba kuna watu wakitaka visa wanakaa saa mbili tofauti na nchi zingine duniani ambako visa huchukua dakika 45 hadi saa moja.

“Hali mbaya pia kwenye mipaka yetu kwa watu ambao wanatumia magari maofisa uhamiaji wamekuwa wakigonga mihuri ya visa bila kuhakikisha taarifa maalum,” alisema.

Naye Mbunge wa Magomeni (CCM), Jamal Kassim, alisema ofisi ya CAG ilikwenda kufanya uchunguzi katika uwanja huo na kubaini kuwa kati ya wageni 65 walioingia nchini, 20 hawakukuwa na taarifa za visa.

Alisema kuna udhaifu mkubwa katika udhibiti na ulipaji wa visa hali inayosababisha mapato ya serikali kupotea.

Akijibu hoja hizo, Kamishna wa Fedha na Utawala wa Uhamiaji, Edwar Chogero, alikiri kuwapo changamoto kwenye visa nchini.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa kikao, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, Japheth Hasunga, alimwagiza Ofisa Masuhuli (Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) kuimarisha mfumo wa udhibiti upotevu wa fedha katika mapato yanayotokana na visa.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Catherine Ruge, alisema kuna mtumishi wa idara hiyo alilipwa Sh. milioni 9.3 kwa ajili ya ununuzi wa fulana na vitu vingine, lakini hadi leo hakuna vitu ambavyo vimepokewa katika orodha ya mali hizo.

Alihoji ni sheria gani imetumika kumlipa fedha taslimu na kwamba hakuna sheria inayoruhusu mtumishi kulipwa zaidi ya Sh. milioni tano.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Projest Rwegasira, alisema ni kweli taratibu za ununuzi zilikiukwa na wameanza kumshughulikia kwa kukata sehemu ya fedha katika mshahara wake mwezi huu.

Source: Mtanzania

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017