Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Ufafanuzi Manji kuvuliwa Udiwani

Manji kwa sasa anasota rumande akikabiliwa na kesi mbili ambazo zote zinasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Kesi ambazo anakabiliwa nazo ni ya matumizi ya dawa za kulevya na uhujumu uchumi.

Wakati akipambana kujinasua na kesi hizo, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jana ilipigilia msumari mwingine kwa Manji, baada ya kutamka kumvua nafasi ya udiwani kwa maelezo ya kukiuka kanuni na sheria za udiwani.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meya wa Manispaa hiyo, Abdallah Chaurembo, alitoa sababu ambazo zimesababisha kumvua udiwani wa Kata ya Mbagala Kuu, ni kutohudhuria vikao vitatu mfululizo.

Vikao ambavyo hakushiriki ni vile vilivyofanyika Machi 3-4, Mei 18-19 na Agosti 24 na 25, mwaka huu.

Chaurembo alisema hatua hiyo ya Manji ya kutoonekana katika vikao, imevunja kanuni za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke zilizoundwa mwaka 2015.

Alisema kwenye kanuni hiyo, kifungu cha 72(C), kinatamka diwani pamoja na majukumu mengine aliyonayo, lazima ahudhurie mikutano ya Halmashauri na kamati ndogo ambayo yeye ni mjumbe bila kukosa.

Aidha, katika Sheria ya Serikali za Mitaa sura ya nane ya mwaka 1982, kifungu cha 25(5)- (a) na (b) kimeainisha ukomo wa udiwani kwa kusema mjumbe wa Baraza la Madiwani ambaye hakuhudhuria vikao vitatu mfululizo bila kutoa taarifa yoyote ya maandishi kwa Mwenyekiti atakuwa amejiondoa katika nafasi hiyo.

“Nasikitika kusema kwamba aliyekuwa Diwani wa Mbagala Kuu, Yusufu Manji, amezivunja kanuni na sheria hizi kwa kutohudhuria vikao na kutoandika barua zenye vielelezo,” alisema Chaurembo.

Aliongeza; “Pia amevunja kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke za mwaka 2015, kifungu cha 73 (1) ambazo zinaeleza wazi kuwa kiti cha mjumbe wa Halmashauri kitakuwa wazi endapo mjumbe bila sababu ya kuridhisha au bila idhini au kibali cha maandishi cha mwenyekiti, atakosa kuhudhuria mikutano mitatu.”

Alisema kutokana na nafasi yake na mamlaka aliyopewa kisheria na kikanuni, imemlazimu kutengua nafasi hiyo ya diwani wa Kata ya Mbagala Kuu.

Meya Chaurembo, alisema ameshamwandikia barua yenye viambatanishi ya utenguzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, ikielezea undani wa hatua hiyo, ili taratibu zingine zifuate.

Hata hivyo, Meya huyo alisema kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo, walijaribu kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwasiliana na Manji kutaka kujua kwa nini haonekani katika vikao.

Alisema ndipo Februari 20, mwaka huu, Manji aliwasilisha barua kwa Mkurugenzi, akieleza hatoweza kuhudhuria vikao kutokana na kuwa na matatizo ya kiafya.

Hata hivyo, alisema barua hiyo yenye kumbukumbu namba YM-MBGKUU/51/2017 haikuambatanishwa na uthibitisho wa daktari.

Machi 22 mwaka huu, Mkurugenzi alimwandikia barua nyingine yenye kumbukumbu TMC/MD/K.11/58/57,  akimtaka awasilishe taarifa za kidaktari kuthibitisha matatizo yake ya kiafya kama alivyoeleza kwenye barua yake.

Mei 22, lakini Manji aliandika barua yenye namba YM/MBGKUU/64/2017, akieleza sababu kama za awali za kutohudhuria vikao vya Halmashauri.

Safari hii aliweka wazi nia yake ya kutaka kujiuzulu endapo afya yake haitaimarika.

Wakati mawasiliano hayo ya barua yakifanyika, Chaurembo alisema Manji hakuhudhuria vikao vya kamati ambavyo yeye ni mjumbe vilivyofanyika Februari 3, Machi 24, Juni Mosi, Agosti 25 na Novemba 24 mwaka jana. Pia, hakutokea katika vikao kama hivyo vya Februari 14 na 15 mwaka huu.

Vikao vingine ambavyo alikuwa mjumbe na hakuhudhuria ni vya Machi 18, Agosti 17, Novemba 8 mwaka jana na Februari 11, mwaka huu.

“Vikao vyote hakuhudhuria na alishindwa kuthibitisha taarifa zake za ugonjwa, huku ni kuvunja kwa makusudi kanuni za Halmashauri pamoja na sheria ya Serikali za Mitaa.

Amekosa sifa ya kuendelea kuwa Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu na kata hii itangazwe kuwa iko wazi,” alisema Meya Chaurembo.

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017