Like Us On Facebook
Follow Us on Twitter

Ukawa Watoa Neno Magari ya Makonda

Ukawa Watoa Neno Magari ya Makonda

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Maalim Seif Shariff Hamad, Julius Mtatiro ametaka magari ya polisi ambayo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alikabidhiwa jana yatumike kutimiza haki badala ya kukandamiza.

Akizungumza na Nipashe baada ya Makonda kukabidhiwa magari 16 yaliyokarabatiwa na kufanana na ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UN), Mtatiro ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kijamii alisema:

“Kukabidhiwa magari Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ni jambo moja lakini namna ya kuyatumia ni jambo jingine.”

Mtatiro ambaye chama chake ni moja ya vinavyounda mwavuli wa kisiasa wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema magari hayo yatapaswa kutumika kukabiliana na uhalifu badala ya kudhibiti harakati za kisiasa, kwa mfano.

Mbali na CUF, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni Chadema, NSSR Mageuzi na NLD ambavyo kwa pamoja viligawana majimbo na kuweka mgombea mmoja wa urais, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Uongozi wa Mtatiro, ambaye ni wa kambi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, upo katika mvutano mkali na Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba, anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hata hivyo.

Aidha, Mtatiro alisema vyombo vya usalama nchini bado vina uhitaji mkubwa wa vifaa na vitendea kazi, hivyo hafla ya jana ni jambo jema.

Alitaka upatikanaji wa vitendea kazi kuwa mkakati wa nchi, badala ya mkoa.

Makonda, kwa jithada zake binafsi katika kuboresha mazingira ya kazi ya polisi wa mkoa wake aliomba kukarabatiwa na kubadilishwa mwonekano wa magari 58 chakavu ya polisi kwa karakana moja binafsi iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro, mwaka jana.

"Ninachoamini pia ni kwamba kuna tatizo kubwa la upungufu wa vitendea kazi vya ulinzi nchi nzima, hivyo ni vema ukawekwa mkakati maalum na Waziri wa Mambo ya Ndani, kuhakikisha vitendea kazi vya kutosha vinapatikana hasa katika eneo la upelelezi, isiishie tu kwenye magari," alisema Mtatiro.

Makonda alikabidhiwa magari hayo katika hafla iliyofanyika Moshi, kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii zilizopatikana jijini.

Hafla ya kukabidhi magari hayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.
Magari hayo yatakuwa na uwezo wa kubeba askari tisa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makonda alisema kupatikana kwa magari hayo kutasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa kuwa yana uwezo wa kuwasaidia askari kukabiliana na wahalifu.

Alisema magari hayo yatatumika kufanyia doria saa 24 katika mkoa wake kwa ajili ya kuhakikisha polisi wanapambana na vitendo vya uhalifu. 

Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka

===

Tupe Maoni Yako Hapa Chini
 

Mawingu Blog | Home Of Newz Copyright © 2017