Shirika la Afya Dunia (WHO) limetengua uteuzi wa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kuwa Balozi Mwema wa Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) barani Afrika kutokana na malalamiko ya watu mbalimbali wakielezea kutoridhishwa na uteuzi huo.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya shirika hilo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhano amesema kuwa, kwa siku chache zilizopita, nimefiriki kuhusu uteuzi wangu wa Mhe. Mugabe kama balozi mwema, na baada ya kutafakari kwa kina, nimeamua kutengua uteuzi huo.
"Nimesikiliza kwa kina mawazo ya wote walioeleza kuhusu kutoridhishwa kwao na uteuzi huo, na nimesikiliza madai mbalimbali yaliyoibuliwa. Pia nimewasiliana na serikali ya Zimbabwe, na tukafikia kwenye hitimisho kuwa uamuzi huu ni bora kwa manufaa ya shirika letu, "aliandika Tedros Adhano.
Baadhi ya watu waliokosoa uteuzi huo wa Rais Mugabe walisema kuwa, katika kipindi cha miaka 30 cha uongozi wa Rais Mugabe, mfumo wa afya wa taifa hilo umeporomoka pakubwa.
Wakosoaji walisema kuwa hospitali hazina dawa, watumishi wa afya wakati mwingine hawalipwi stahiki zao, na kiongozi huyo aliyekaa madarakani tangu uhuru, husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Licha ya kutengua uteuzi huo, Tedros amesema kuwa, bado yupo kwenye nafasi ya kufanya kazi na nchi yeyote na kwamba wapo tayari kushirikiana na mtu yeyote katika kujenga mfumo wa afya ulio imara.
Aidha, amewashukuru wote waliotoa mawazo yao kuhusu uteuzi huo na kusema kuwa, anategemea ana mijadala ya kujenga ili kuweza kutekeleza majukumu aliyochaguliwa kuyafanya.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini