Mashabiki wa klabu ya soka ya Yanga wamebaki kwenye sintofahamu endapo mwenyekiti wao wa zamani Yusuf Manji amerejea kwenye madaraka yake au la.
Kupitia ukurasa rasmi wa klabu hiyo kwenye mtandao wa Instagram imewekwa picha yenye utata ikielezea kuanza kuuzwa kwa jarida la klabu hiyo linaloitwa ‘Yanga Magazine’,wakati ukurasa wa pili wa Jarida hilo ukiwa na ujumbe unaoashiria kurejea kwa Manji ndani ya Yanga.
Katika ukurasa huo wa pili wa Jarida hilo yameandikwa maneno haya “SHUJAA AMERUDI SHUJAA YUPO NYUMBANI” huku yakipambwa na picha ya mfanya biashara huyo ambaye alijiuzulu cheo hicho miezi kadhaa iliyopita.
Kama hiyo haitoshi inaonekana kuna Makala ambayo ina maelezo ya maneno hayo japo yametiwa kivuli kiasi kwamba hayawezi kusomeka kwa urahisi. Swali linabaki kuwa Je, kuelekea pambano la watani wa Jadi Yanga na Simba siku ya jumamosi huenda Manji akatangaza kurejea kuiongoza Yanga?
Yanga na Simba zitakutana kwenye mechi ya raundi ya nane siku ya jumamosi kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam. Hadi sasa timu hizo zinalingana pointi kila mmoja akiwa na 15 baada ya mechi saba huku Simba ikiongoza kwa tofauti ya mabao.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini