WAKATI sakata la ‘ndoa’ ya msanii wa Bongo Fleva, Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ na mwigizaji Irene Pancras Uwoya likizidi kupamba moto, mashehe mbalimbali wameibuka na kutoa sababu zinazodhihirisha kuwa ndoa hiyo ni batili, Ijumaa Wikienda linakupakulia ubuyu wa motomoto.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Ijumaa Wikienda, mashehe watatu wa misikiti tofauti jijini Dar, walioomba hifadhi ya majina, walimkosoa Uwoya na Dogo Janja kwa kuonesha kwamba walichokifanya si sahihi.
NI BATILI
Mashehe hao walisema kuwa, ndoa hiyo ni batili kutokana na jinsi ilivyofungwa, lakini pia hata kama walikuwa wanafanya filamu, bado walikiuka taratibu za Dini ya Kiislam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa mashehe hao alianika sababu tano (5) zinazodhihirisha kwamba ndoa hiyo ni batili;
SABABU YA KWANZA (MATITI NJE)
Alisema kuwa, katika picha mbalimbali zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Uwoya akiwa amevaa gauni la harusi, zinamuonesha akiwa matiti nje, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa bibi harusi wa Kiislam kuacha nje maumbile hayo nyeti ya mwanamke yanayopaswa kusitiriwa mbele ya kadamnasi.
“Dini yetu hairuhusu kabisa mwanamke kuacha matiti wazi wakati wa kumfungisha ndoa,” alisema shehe huyo.
SABABU YA PILI (KUACHA KICHWA WAZI)
Shehe huyo aliitaja sababu ya pili kuwa, ni kitendo cha Uwoya kuonekana akiwa amevaa ‘less wigi’ huku akiwa ameacha kichwa wazi, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa dini hiyo wakati alidai kwamba, alibadili dini na kuwa Muislam kisha kupewa jina la Sheila.
“Unaanzaje kufungishwa ndoa ukiwa na liwigi lako kichwani? Pale panaonesha kabisa hata kama walikuwa wanafanya filamu, basi walishindwa kujielimisha kisawasawa,” alisema shehe huyo.
SABABU YA TATU (TATUU)
Shehe huyo alisema kitendo cha mrembo huyo kuonekana kwenye picha hizo za ndoa akiwa na tatuu mbalimbali mwilini ikiwemo ile ya msalaba alijichora mgongoni kwa juu, kilizidi kuwakera zaidi watu kwamba wawili hao hawakuwa ‘serious’ katika kile walichokuwa wakikifanya kwani hakuna shehe anayeweza kukubali kuwafungisha ndoa watu wakiwa katika mwonekano huo.
“Ule ni mzaha kabisa walikuwa wanafanya, mtoto wa kike umejichora tatuu halafu tena zinaonekana wazi kabisa halafu shehe aridhie tu mfunge ndoa? Utani ule,” alisema shehe huyo kwa ukali.
SABABU YA NNE (CHETI)
Kama hiyo haitoshi, shehe huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema, ndoa hiyo inakosa uhalali kwani hata kama ni kiki kama vile alivyokiri Uwoya kwamba ni filamu, hairuhusiwi kufanyia mchezo vyeti vya ndoa kwa kuwa viko kimahesabu na huwa vinapelekwa BAKWATA kwa ajili ya kumbukumbu ya ndoa zilizofungwa.
SABABU YA TANO (KUFUNGA NDOA SEHEMU MOJA)
Shehe huyo alimaliza na sababu ya tano kwa kusema, wawili hao wanaonekana wakifunga ndoa sehemu moja, tofauti na taratibu za ndoa nyingine za Kiislam kwani mwanaume huanza kufungishwa ndoa nje akiwa amezungukwa na wanaume wenzake huku bibi harusi akiwa chumbani, lakini kwao ilikuwa ni tofauti.
“Hapo ndipo utagundua kabisa kwamba hakuna ndoa pale. Unaanzaje kumfungisha halafu eti wote wanasaini cheti cha ndoa hapohapo pamoja, haipo hiyo Kiislam,” alisema shehe huyo na kuongeza:
“Licha ya hivyo, wazazi wa pande zote nimeambiwa hawakuwepo na walioshika nafasi hizo ni wasanii wenzao, jambo ambalo linaonesha kabisa siyo ndoa halali.”
MSIKIE MTABIRI MAARUFU
Akizungumzia ndoa hiyo mtabiri maarufu Bongo, Maalim Hassan Yahya alipigilia msumari kuwa ndoa hiyo ni batili kwani kwa utaratibu wa Dini ya Kiislam, bibi harusi hawezi kukaa nusu utupu yaani matiti nje kama ilivyokuwa kwa Uwoya.
Aidha, alisema kuwa, utaratibu uliotumika siyo sawasawa na kama ni kiki, basi Dogo Janja atakuwa amemkufuru Mungu na ipo siku Mungu atamwadhibu maana ndoa ni jambo takatifu, lakini amelifanyia utani na kuwadanganya watu kuwa ameoa.
“Yaani atakuwa amemkufuru Mungu kama ndiyo hizo kiki zao wanazozifanya. Kuna mambo ya kufanyia mzaha, lakini si suala kama hili linalogusa imani,” alisema Maalim.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini