Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ametoa tamko la kulaani uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ambayo imemuagiza mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi dhidi ya mgogoro wa Burundi.
Rais Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema ICC inaingilia mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kuwahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo jambo ambalo sio sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.
Rais Museven amezungumza hayo kabla ya kuagana na Rais Magufuli ambaye jana amemaliza ziara rasmi ya kiserikali ya siku 3 nchini Uganda na kurejea nchini Tanzania.
Akizungumzia uamuzi huo wa ICC Mh. Magufuli amesema hatua hiyo inarudisha nyuma hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo iliunda Kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Mhe. Rais Museveni na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa.
Rais Magufuli aliagana na Rais Museveni katika Mji wa Masaka na baadaye kusindikizwa na Makamu wa Rais wa Uganda Mhe. Edward Kiwanuka Sekandi hadi Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini