Mahakama ya Wilaya ya Arusha imemuachia huru Diwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga baada ya kukutwa hana hatia katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili ya kuhamasisha maandamano ya UKUTA.
Bananga alishtakiwa kwa kutoa maneno ya uchochezi, mwezi Agosti mwaka jana akiwa wilayani Monduli akidai kuwa ATAWASHIKISHA UKUTA VIONGOZI WA CCM NA SERIKALI ifikapo Septemba 1 mwaka jana ambapo ilikuwa siku ya kuzindua oparesheni UKUTA nchi nzima.
Upande wa Jamhuri uliieleza mahakama kuwa maneno ya Bananga kwamba atawashikisha ukuta viongozi serikali ni udhalilishaji na ni uchochezi maana yanahamasisha wengine kufanya hivyo.
Awali Wakili wa upande wa utetezi, Shecky Mfinanga alimuuliza askari polisi aliyekuwa anatoa ushahidi kama anafahamu ukuta. Askari huyo alisema anaufahamu.Wakili Mfinanga alimtaka askari huyo ashike ukuta wowote katika mahakama hiyo ili kudhibitisha kama anaujua. Askari huyo akashika.
Mfinanga akamuuliza kama amedhalilika. Askari huyo akasema hajadhalilika. Mfinanga akamuuliza ikiwa yeye ameshika ukuta na hajadhalilika, iweje Bananga kuwashikisha ukuta viongozi wa serikali na wa CCM iwe udhalilishaji? Askari huyo alishindwa kujibu.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Devotha Msofe amesema kuwa upande wa Jamhuri umefanya kosa kumfungulia Bananga kesi wilayani Arusha kwa kosa analodaiwa kulifanya wilayani Karatu
Hivyo Mahakama hiyo imemuachia huru Bananga baada ya kukosa ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini