Usiku wa kumkia leo( saa saba usiku) Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngalamgosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa Bw. Felix amesimmisha kazi kuanzia leo Juni 11, 2017.
Maamuzi haya yamekuja siku mbili baada ya habari za kampuni ya IPTL kutaka kuongezewa mkataba wa uzalishaji umeme ambapo pia Kituo cha sheria na haki za Binadamu kilijitokeza na kusema hakikubaliani na mkataba huo kuongezwa kwani kampuni hiyo inahusishwa na kashfa ya uchotwaji wa Mabilioni kupitia account ya ESCROW.
Rais Magufuli huko nyuma amewahi kusikika akiuponda mkataba wa IPTL na kusema kuwa ni mkataba wa hovyo unaopelekea kutokuwapo kwa umeme wa uhakika kutokana na watu hao kufanyabiashara bila kujali utoaji huduma.
“Ni lazima nchi yetu tuachane na umeme usio na uhakika, umeme wa kukodishakodisha, umeme wa kutumia watu na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi mara IPTL, mara nini, ni kwa sababu tulizoea maumeme ya kukodisha kodisha, ya wafanyabiashara,” alisema Rais Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II.
Rais Magufuli alisema kuwa ni lazima Tanzania iachane na mitambo ya kukodi na TANESCO ijiwekee mikakati ya kuzalisha umeme wake yenyewe ili kutoa huduma ya uhakika kwa wananchi.
“Tuachane na mitambo ya kukodi, tumechoka kufanyishwa biashara na wawekezaji, tunalipia `capacity charge’ za ajabu ajabu halafu tunalipia bei ya ajabu. Tunawapa shida Watanzania wa hali ya chini, kila mmoja anahitaji umeme, lakini wengine wanashindwa kuuvuta kwa sababu umeme ni wa juu.”
Kutokana na kauli hiyo ambayo Rais Magufuli aliitoa Machi 2016 ni dhahiri kuwa serikali isingekuwa tayari kuendelea na mkataba na IPTL ambayo yeye anaamini kuwa inawanyonya watanzania.
Juni 7 mwaka huu EWURA ilitangaza kupokea maombi ya IPTL ikiomba kuongeza muda wa leseni uweze kuendana na mkataba wa mauziano ya umeme na TANESCO.
EWURA ilisema kuwa imeyapitia maombi hayo na kuwa inadhamiria kuiongezea muda kampuni hiyo kutokana na makubaliano ya kuuziana umeme yaliyopo kati ya IPTL na TANESCO
EWURA iliwataka wanachi na wadau mbalimbali kutoa maoni yako kuhusu kusudio hilo ambapo wengi waliotoa maoni hayo walipinga kusudio la IPTL kuongezewa muda wa leseni yake.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliitaka EWURA kuondoa kusudio la kuiongezea muda IPTL na pia kuwaomba msamaha wananchi na wabunge.
IPTL ilikuwa ikiomba kuongezewa muda wa miezi 55 ya kuendelea na biashara ya kuiuzia umeme TANESCO kuanzia Julai 17, 2017 hadi Januari 15, 2022 ambapo ni miaka minne na nusu.
Bonyeza HAPA Kudownload Applicationi Ya Mawingu Blog Kwenye Simu Yako Ili Kupata Habari Zetu Haraka
===
Tupe Maoni Yako Hapa Chini